Swali: Ametaja Shaykh katika maneno yake kuwa haijuzu kuondoa maovu kwa maovu makubwa zaidi. Je, inajuzu kutoka dhidi ya mtawala ambaye ameacha kutekeleza adhabu za kidini, akafungua baa, akawafunga waislamu na akazuia ujenzi wa misikiti? Namaanisha kumuua mtawala?

Jibu: Hili alilolitaja ni kanuni ya Kishari´ah: haijuzu kukataza maovu ikiwa kunapelekea maovu makubwa zaidi. Ikiwa kumkemea mtu anayekunywa pombe au kufanya maovu mengine kunasababisha shari kubwa zaidi, kama kuuawa au madhara makubwa, basi huachwa ili kuepuka lililo baya zaidi. Vivyo hivyo kuwaua watawala na viongozi, Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amekataza kufanya uasi dhidi yao, kwa sababu kuwaua kunasababisha fitina kubwa zaidi, vurugu, kuuawa kwa wasio na hatia na mengineyo. Walipomlalamikia kuhusu viongozi wanaofanya maasi ambapo wakauliza:

“Je, tusiwapige vita?” Akasema: “Hapana, muda wa kuwa wanasimamisha swalah miongoni mwenu. Isipokuwa mtapoona ukafiri wa wazi mlio nao ushahidi kutoka kwa Allaah.”

Akasema tena (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Wapeni haki zao na muombe Allaah haki yenu.”

“Yeyote atakayebeba silaha dhidi yetu si miongoni mwetu.”

“Yeyote atakayekujieni na hali yenu ni moja ambapo anataka kuvunja umoja wenu, basi muueni yeyote atakayekuwa.”

Kwa hiyo kutoka dhidi ya watawala haijuzu ikiwa kunasababisha fitina na shari au ikiwa hawajaonyesha ukafiri wa wazi. Lakini ikiwa wameonyesha ukafiri wa wazi na kuna uwezo mkubwa wa kumuondoa kiongozi huyo na kuweka badala yake mwingine bora zaidi bila kusababisha madhara kwa waislamu, basi hilo lina nafasi yake. Ama yale yanayofanywa na baadhi ya watu ya mauaji ya kisiri na maovu yanayosababisha uharibifu kwa waislamu, hilo ni maovu. Haijuzu. Huku ni kuondoa maovu kwa kufanya maovu makubwa zaidi na mabaya zaidi. Kwa hivyo haijuzu.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3515/حكم-الخروج-على-حاكم-لم-يطبق-الشرع
  • Imechapishwa: 26/11/2026