Masuala ya saba: Kusoma Qur-aan kwenye makaburi. Tunasema – na Allaah ndiye anajua zaidi – ya kwamba wanachuoni wametofautiana katika kauli tatu na kuna mapokezi matatu pia kutoka kwa Imaam Ahmad:

Ya kwanza: Imechukizwa pasina kufungamana kwa msemo mwingine ni haramu. Haijuzu kusoma Qur-aan kwenye makaburi. Katika hili kuna upokezi mmoja kutoka kwa Imaam Ahmad. Hii ndio kauli ya Abu Haniyfah na Maalik. Dalili zao ni hizi zifuatazo:

1- Kusoma Qur-aan kwenye makaburi ni tendo lililozushwa na halikuthibiti katika Sunnah. Haikuthibiti kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisoma kwenye makaburi au aliamrisha kufanya hivo.

2- Kisomo ni kama swalah. Kisomo kimefanana na swalah na kuswali kwenye makaburi kumekatazwa.

3- Asli katika ´ibaadah ni kujizuia na kukomeka mpaka kupatikane dalili zenye kuonesha kuwa inajuzu.

4- Kisomo ni njia inayopelekea katika kufanya I´tikaaf kwenye kaburi na kuliadhimisha. Hivyo imekatazwa ili kuziba njia ya shirki.

Ya pili: Kujuzu kusikofungamana. Makusudio hapa ni kabla ya kuzika au baada ya kuzika. Kuna upokezi mmoja juu ya hili kutoka kwa Imaam Ahmad na ni kauli ya Muhammad bin al-Hasan mtu wa pili wa Abu Haniyfah na ametumia hoja kutokana na yaliyonukuliwa kutoka kwa Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ambaye aliusia kusomwe kwenye kaburi lake wakati wa kumzika kwa kupitwa na Suurat-ul-Baqarah na kutoikhitimu . Imenukuliwa vilevile kutoka kwa baadhi ya Muhaajiruun kusoma Suurat-ul-Baqarah na kusema ni ukurubisho na ndani yake mna du´aa. Hili ni pamoja na kwamba dalili imekhusishwa tu wakati wa kuzika tofauti na watu hawa wametanua zaidi na kujuzisha kisomo pasina kufungamana wakati wa kuzika na baada yake.

Ya tatu: Kujuzu wakati wa kuzika na machukizo baada yake. Kuna upokezi mmoja juu ya hili kutoka kwa Imaam Ahmad. Dalili ya wenye kauli hii ndio dalili zile zile za watu wenye kauli ya pili. Nayo ni yale yaliyonukuliwa kutoka kwa Ibn ´Umar na baadhi ya Muhaajiruun. Hii ndio kauli ambayo Ibn Abil-´Izz ambaye amesherehesha “at-Twahaawiyyah” ameipa nguvu na kusema kuwa ndani yake mna kuoanisha baina ya maoni yote mawili.

Kauli ya sawa ni ile ya kwanza. Watu wenye madhehebu ya pili na ya tatu wanajibiwa kama ifuatavyo:

1- Nukuu hii kutoka kwa Ibn ´Umar kwanza inahitajia kuthibiti. Kadhalika yaliyopokelewa kutoka kwa baadhi ya Muhaajiruun.

2- Tukikadiria kweli kama imesihi kutoka kwa Ibn ´Umar basi kunasemwa kuwa hili ni kutokana na Ijtihaad yake. Kuna Maswahabah wengine walioenda kinyume na Ibn ´Umar. Hivyo basi kauli yake si hoja. Kuna Maswahabah wakubwa wameenda kinyume naye, kwa mfano Abu Bakr, ´Umar na wengine. Hili ikiwa kweli nukuu hii imesihi kutoka kwa Ibn ´Umar. Na Allaah ndiye anajua zaidi.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah ar-Raajhiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Hidaayah ar-Rabbaaniyyah fiy Sharh al-´Aqiydah at-Twahaawiyyah (02/727-729)
  • Imechapishwa: 18/05/2020