Swali: Ikiwa mtu amesoma Qur-aan, kisha akatoa thawabu zake kwenda kwa baba yake au kwa rafiki yake au kwa ndugu yake. Je, thawabu hizo humfikia?

Jibu: Kuna tofauti ya mitazamo kati ya wanazuoni. Baadhi ya wanazuoni wamesema kuwa ikiwa mtu ametoa thawabu, basi thawabu zinamfikia. Huu ni msimamo wa wengi miongoni mwa wanazuoni. Wengine wakasema kwamba haikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kutoka kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) kwamba walifanya hivyo. Kwa hiyo lililo bora kwake ni kuacha. Lakini swadaqah na du´aa – hivi viwili ndivyo vilivyo bora zaidi – kwa idhini ya Allaah. Hakuna haja ya kusoma Qur-aan. Kila mtu asome kwa ajili ya nafsi yake, asome na thawabu ziwe kwa ajili yake mwenyewe, kwa sababu haikuthibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala kutoka kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum) kwamba walifanya hivyo. Hivyo kilicho bora ni kutokifanya.

Lakini mtu akitoa swadaqah kwa niaba ya maiti – kwa mali au kwa chakula – hayo ndio yanayomnufaisha maiti kwa maafikiano ya waislamu. Vivyo hivyo du´aa mahali popote kwa ajili yake ya kupata msamaha na rehema humfaa.

Ama kumzawadia swalah yake au kisomo chake cha Qur-aan, hakuna dalili juu ya hilo. Vivyo hivyo ikiwa mtu amekufa na anadaiwa funga na hakufunga hali ya kuwa afya yake ishakuwa vizuri, lakini akapuuzia na hakufunga, basi afungiwe na walii au jamaa zake, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mwenye kufa na ana deni la swawm, basi atafungiwa na walii wake.” 

Vivyo hivyo ikiwa amekufa na ana wajibu wa Hajj ya faradhi na hakuwahi kuhiji au ana deni la Hajj ya nadhiri, basi ahijiwe.

Kuhusu swalah, haswaliwi. Hilo ni jambo ambalo halikupokelewa. Hakuswaliwi kwa niaba ya maiti. Hilo ni jambo halina msingi.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1141/هل-يصل-ثواب-قراءة-القران-للميت
  • Imechapishwa: 09/06/2026