Sura hiyo haikuwahi kutokea kipindi cha Salaf

Swali: Je, inafaa kuongozwa katika swalah na ambaye amekuja amechelewa na yuko analipa swalah yake?

Jibu: Hapana, haijuzu. Kwa sababu jambo hilo halikutokea katika zama za Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) wala katika wakati wowote wa Salaf.

 al-Bukhaariy amepokea katika ”as-Swahiyh” yake kwamba asubuhi moja Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alitoka kukidhi haja na kipindi hicho alikuwa na al-Mughiyrah bin Shu´bah. Pindi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipotaka kutawadha basi al-Mughiyrah akawa anammwagilia maji huku anatawadha. Wakati wote huo watu walikuwa wanamsubiri ili aweze kuwaongoza katika swalah. Pindi walipoona kuwa amechelewa wakamtanguliza mbele ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf aswalishe. Akaja al-Mughiyrah akiwa pamoja na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). al-Mughiyrah akataka imamu arudi nyuma na ampe nafasi Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), lakini akamwashiria amwache. Hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na al-Mughiyrah wakamfuata ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf. ´Abdur-Rahmaan bin ´Awf alipotoa salamu wakasimama na kulipa ile Rak´ah ambayo ilikuwa imewapita. Katika hali hii al-Mughiyrah hakumfuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ili kukamilisha swalah hii, tofauti na wanavofanya baadhi ya watu hii leo.

Vilevile sura ambayo umeitaja punde kidogo, nayo ni kwamba anakuja mtu ambaye amechelewa swalah ya mkusanyiko na anawakuta watu ambao wamekuja wamechelewa ambao wako wanalipa swalah zao ambapo akawafuata. Hili ni jambo ambalo halikuwahi kutokea hata siku moja.

  • Mhusika: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa Raabigh (6)
  • Imechapishwa: 20/12/2020