Sujuud ya kisomo na ya kushukuru kwa mwenye janaba, hedhi au nifasi

Swali: Je, inafaa kwa mwanamme au mwanamke mwenye janaba kusujudu kwa ajili ya Sujuud ya kisomo?

Jibu: Wanazuoni wametofautiana juu ya sijda ya kisomo na sijda ya kushukuru; imeshurutisha kuwa na twahara kutokamana na hadathi mbili? Kuna maoni mawili na sahihi zaidi katika maoni hayo mawili ni kwamba haikushurutishwa. Hakuna dalili juu ya hilo. Sujuud peke yake sio swalah na wala haina hukumu ya swalah. Lakini ni sehemu ya swalah. Kwa hivyo haikushurutishwa twahara. Ni kama mfano wa aina nyenginezo za Dhikr tukitoa Qur-aan.

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akisoma Qur-aan na anapopita katika sijda basi anasujudu na Maswahabah zake wanasujudu pamoja naye. Haikuthibiti kutoka kwake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba aliwaamrisha kujitwahirisha juu ya jambo hilo. Kama inavotambulika vikao vinakusanya walio na janaba na wasiokuwa na janaba. Kama twahara ingelikuwa ni sharti kwa ajili ya Sujuud kutokamana na hadathi kubwa au hadathi zote mbili, basi angelibainisha Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Haijuzu kuchelewesha ubainifu wakati wa haja. Ni kama ambavo yeye (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alibainisha kwa matendo na maneno yake ya kwamba haifai kwa mwenye janaba kusoma Qur-aan.

Kwa hivyo kunakuwa wazi kufaa kwa mwenye janaba, mwenye hedhi na waislamu wengineo wasiokuwa na twahara kusujudu sijda ya kisomo na sijda ya kushukuru. Haya ni kutokana na maoni sahihi zaidi ya wanazuoni.

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (11/412)
  • Imechapishwa: 16/11/2021