Muulizaji swali ni Abul-Fadhwl Qaasim Mafuta:

Sisi tuna baadhi ya vikwazo katika Da´wah. Tatizo kubwa linalotukabili ni Suruuriyyuun. Mtandao wa Muhammad Suruur una ushawishi na walinganizi wengi nchini Tanzania na Kenya. Watu wa kwanza waliokuwa wakitupiga vita, wakituraddi na kutuchafua ni Suruuriyyuun kabla ya Suufiyyuun. Walichoanza ni kutadharisha watu na sisi wakiwaambia watu kuwa sisi ni ´as-Salafiyyah al-Jadiydah` na kwamba sisi tumekuja na mambo mepya, tunawakufurisha watu na kuwafanyia Tabdiy´ na Tafsiyq. Matokeo yake wakazua neno hili ´as-Salafiyyah al-Jadiydah`. Kwa mujibu wao wao ndio Salafiyyah wa kihakika.

Kwanza tulikuwa tunataka utuwezee wazi chanzo cha msemo huu ´as-Salafiyyah al-Jadiydah`. Tukisoma baadhi ya vitabu ikiwa ni pamoja vilevile na kitabu “Fataawaa al-Jaliyyah” cha Shaykh Ahmad an-Najmiy (Rahimahu Allaah) aliulizwa swali hili kama kuna ´as-Salafiyyah al-Jadiydah` na ´as-Salafiyyah al-Qadiymah` ambapo akasema kuwa hakuna as-Salafiyyah al-Jadiydah[1]. Lakini hata hivyo tulikuwa tunapenda kujua chanzo cha msemo huu ulianzia wapi na kama kuna mgongano katika sentesi hii “as-Salafiyyah” halafu “al-Jadiydah” au ni sentesi sahihi kwa mujibu wa lugha ya kiarabu.

´Allaamah Rabiy´ al-Madkhaliy akijibu:

Kwanza ninamuomba Allaah atuonyeshe sisi na nyinyi haki kuwa ni haki na atujaalie kuweza kuifuata, na atuonyeshe batili kuwa ni batili na atujaalie kuweza kuiepuka.

Ninavyojua ni kuwa watu hawa ambao wanawaelezeni kwa wasifu huu ´as-Salafiyyah al-Jadiydah`, uhakika wa mambo hii ndio sifa yao. Kwa sababu wao ndio wamezua katika Uislamu kwa kuingiza mambo mepya na kuingiza madhehebu ya Khawaarij, kuwapenda Ahl-ul-Bid´ah na kuwatetea katika mfumo wao.

Kuhusu Salafiyyuun wa kihakika ambao wameshikamana barabara na as-Salaf as-Swaalih, sawa inapokuja katika ´Aqiydah na mfumo, na aidha wameshikamana na wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah, mfano wa wanachuoni hao ni kama Ibn Baaz, al-Albaaniy, Ibn ´Uthaymiyn na wenye kufuata uongofu wao katika ulimwengu wa Kiislamu, hii ndio Salafiyyah ya kihakika ambayo nyinyi – Allaah akitaka – mnafuata.

Kwa majaribio ndio hujulikana ni nani Salafiy wa kihakika na Salafiy wa madai. Mfano sisi tunaonelea kuwa Sayyid Qutwub, al-Bannaa na al-Mawduudiy na viongozi wengine wa mapote yaliyopinda ya kwamba wametoka katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hilo ni kutokana na ile misingi na fikira walizounda. Upande mwingine hawa wamesimama upande wao, wamejiunga nao na wanawapiga vita Ahl-us-Sunnah kwa ajili yao. Kasoro inapatikana katika ´as-Salafiyyah` yao – kama wako na hiyo ´as-Salafiyyah yenyewe.

Salafiy [wa kihakika] hawapigi vita wanachuoni wa Ahl-us-Sunnah, jambo ambalo wao wanafanya. Ukiongezea juu ya hilo wanasema kuwa ni vibaraka, majasusi na kwamba ni Murji-ah. Ikiwa nyinyi mna sifa kama hizi, basi ni kweli kwamba ni ´as-Salafiyyah al-Jadiydah`. Na ikiwa hamna sifa kama hizi, basi wao ndio ´as-Salafiyyah` ya madai na sisemi ´as-Salafiyyah al-Jadiydah`, bi maana mpya.

Baadhi yao wanafikia mpaka kuwakufurisha Ahl-us-Sunnah. Tovuti za Suruuriyyah zinawakufurisha Ahl-us-Sunnah. Hili ni jambo linalojulikana kwao. Kwa nini wanafanya hivo? Wanaona kuwa [Ahl-us-Sunnah] ndio Khawaarij.

Leo milipuko hii ugaidi huu uliowatikisa waislamu ni kutokamana na athari ya Da´wah yao. Hilo si kwa jengine ni kwa sababu Da´wah yao imejengwa juu ya fikira za Sayyid Qutwub Takfiyriy. Bali wanatetea mifumo yake mingine ambayo tumeandika kiasi kikubwa juu yake. Mfano wa mifumo hiyo ni kama ya kusema kwamba kila kitu ni Allaah, kwamba Allaah amekita kwenye kila kitu, roho ni kitu cha milele, ujamaa na kuwatukana Maswahabah. Mambo yote haya yanapatikana kwa Sayyid Qutwub. Lakini pamoja na hivyo wanamzingatia kuwa yeye ndio kiongozi wao. Wapeni mtihani kwa kunukuu aliyosema Sayyid Qutwub, Hasan al-Bannaa na al-Mawduudiy katika mambo ambayo yanaenda kinyume na mfumo wa Salaf. Mtapowauliza jisaidieni kwa yale niliyoandika kuhusu Sayyid Qutwub. Kwa mfano anasema juu ya ´Uthmaan bin ´Affaan (Radhiya Allaahu ´anh):

“Uasi dhidi ya ´Uthmaan ilikuwa karibu na roho ya Kiislamu.”

Amesema tena kuhusu uongozi wa ´Uthmaan:

“Uongozi wa ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh) ndio ulistahiki kufuatia baada ya Abu Bakr na ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhuma). Kuhusu uongozi wa ´Uthmaan ilikuwa ni pengo.”

Sivyo tu, bali amewatukana Banuu Umayyah na kufikia mpaka kuwakufurisha. Amewakufurisha hata wale walioingia katika Uislamu baada ya kufariki Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hawazingatii. Amefuata mwenendo wa Raafidhwah inapokuja katika msimamo wa Maswahabah. Bali amefuata mwenendo wa Raafidhwa waliopindukia. Mtu kama huyu ndiye kiongozi wao. Sasa ni kina nani ambao ni ´as-Salafiyyah al-Jadiydah`? Rejea katika kitabu “Matwaa´in Sayyid Qutwub fiy Aswhaabi Rasuuli Allaahi” na “al-´Awaaswim mimmaa fiy kutub Sayyid Qutwub min al-Qawaaswim”. Humo mna makosa tele ya Qutbiyyah na viongozi wa al-Ikhwaan. Kwa mfano al-Bannaa, Sayyid Qutwub, at-Twuraabiy, al-Ghazaaliy, Ghannuushiy, al-Mawduudiy na wengineo. Haya yanabainisha yale mepya waliyozua. Wako na uanasekula, umasoni, uhuru wa dini, umoja wa dini na udugu wa dini. Wana yote haya. Pamoja na haya yote hawa wanawapenda vigogo hawa wenye I´tiqaad kama hizi. Kwa mtazamo huu hawa hawana as-Salafiyyah yoyote ile, si ´as-Salafiyyah al-Jadiydah` wala ´as-Salafiyyah al-Qadiymah`.

Salafiy ni yule mtu anayewafuata as-Salaf as-Swaalih katika ´Aqiydah, ´ibaadah na mfumo wao na vilevile akapenda na kuchukia kwa ajili ya hayo. Wao wanaweza kusifika na kitu katika as-Salafiyyah. Lakini, ni kama nilivyowaambieni zaidi ya mara moja, as-Salafiyyah yao ni kama kitungusumu. as-Salafiyyah haina maana yoyote kwao. Hawapendi na kuchukia kwa ajili yake. Kuhusu sisi tunaipenda as-Salafiyyah kuanzia mambo ya msingi mpaka ya matawi, ´Aqiydah na mfumo. Salafiy ni yule mtu anayefuata yale aliyokuwa akifuata Mtume (Swalla Allaahu ´alayh iwa sallam) na Maswahabah zake.

Salafiyyah ndio pote lililonusuriwa ambalo litaendelea kuwa juu ya haki hali ya kuwa ni lenye kushinda mpaka Qiyaamah kifike. Sisi tunajifakhari kwa Maswahabah, maimamu wa Taabi´uun, maimamu wa uongofu na waliowafuata uongofu wao mpaka hii leo. Kuhusu wao huingia kati ya wao na Salaf I´tiqaad za Sayyid Qutwub, al-Bannaa, Muhamamd Suruur, al-Mawduudiy na wengineo.

Mimi nakuusieni baada ya kuisia nafsi yangu kumcha Allaah na kujifakhari kwa mfumo wa Salaf. Puuzieni tuhuma. Kuna watu waliowatuhumu Mitume (´alayhimus-Swalaatu was-Salaam). Kuna watu wanaowatuhumu Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum), nao ni Raafidhwah. Kuna watu wanaowatuhumu wanachuoni wa Kiislamu ilihali ni maimamu wa Sunnah. Msifikirie kuwa ad-Da´wah as-Salafiyyah itaenda hivi hivi kwa usalama na amani na isifikwe na tatizo lolote na kukabiliwa na mitihani. Sivyo hivyo! Amesema (Ta´ala):

أَمْ حَسِبْتُمْ أَن تَدْخُلُوا الْجَنَّةَ وَلَمَّا يَأْتِكُم مَّثَلُ الَّذِينَ خَلَوْا مِن قَبْلِكُم ۖ مَّسَّتْهُمُ الْبَأْسَاءُ وَالضَّرَّاءُ وَزُلْزِلُوا حَتَّىٰ يَقُولَ الرَّسُولُ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ مَتَىٰ نَصْرُ اللَّـهِ ۗ أَلَا إِنَّ نَصْرَ اللَّـهِ قَرِيبٌ

“Je, mnadhani kwamba mtaingia Peponi na hali bado haijakufikieni [mitihani] kama ya wale waliopita kabla yenu? Iliwagusa [shida za] ufukara na dhara za na wakatetemeshwa mpaka Mtume na wale walioamini pamoja naye wanasema: “Lini itafika nusura ya Allaah?” Tanabahi! Hakika nusura ya Allaah iko karibu.” (02:214)

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Watu wenye kupewa majaribio sana ni Mitume. Halafu wale wenye kufanana na wao.”

Ni lazima kuwepo mitihani katika mfumo wao. Allaah anawapa majaribio wapenzi Wake ili Azinyanyua daraja zao na kuwazidishia ujira wao. Amesema (Ta´ala):

وَلَوْ يَشَاءُ اللَّـهُ لَانتَصَرَ مِنْهُمْ وَلَـٰكِن لِّيَبْلُوَ بَعْضَكُم بِبَعْضٍ

“Na lau Allaah angelitaka angewalipiza kisasi Mwenyewe, lakini ili akujaribuni nyinyi kwa nyinyi.” (47:04)

Allaah ni muweza wa kuwaangamiza wapotevu, sawa katika maakiri na mapote na makundi potevu. Allaah angelitaka angeliwaangamiza na akawastarehesha Ahl-us-Sunnah na wao. Lakini Allaah anawapa mtihani Ahl-us-Sunnah ili abainike ni nani mkweli na asiyekuwa mkweli. Amesema (Ta´ala):

الم أَحَسِبَ النَّاسُ أَن يُتْرَكُوا أَن يَقُولُوا آمَنَّا وَهُمْ لَا يُفْتَنُونَ وَلَقَدْ فَتَنَّا الَّذِينَ مِن قَبْلِهِمْ ۖ فَلَيَعْلَمَنَّ اللَّـهُ الَّذِينَ صَدَقُوا وَلَيَعْلَمَنَّ الْكَاذِبِينَ

“Alif Laam Miym. Je, wanadhani watu kwamba wataachwa [bila kupewa mitihani] kwa kuwa wanasema: “Tumeamini.” basi ndio wasijaribiwe?” Kwa yakini Tuliwajaribu wale wa kabla yao ili Allaah Awatambulishe wale waliosadikisha na ili Awatambulishe waliokadhibisha.” (29:01-03)

Kuweni na subira juu ya mtihani huu. Endeleeni na mlinganie katika Qur-aan na Sunnah kwa mfumo wa as-Salaf as-Swaalih.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: soundcloud.com/user-621373875/4-sheikh-rabii-ibn-haad-almadkhal
  • Imechapishwa: 14/07/2020