Sababu iliyowafanya Raafidhwah kuzusha sherehe ya kuzaliwa kwa Mtume

Miaka miatatu kamilifu hakukuweko kabisa kitu kinachoitwa ´sherehe ya mazazi ya Mtume`. Lau ingelikuwa ni kheri basi wangetutangulia kwalo watanguliaji na waliowafuata kwa wema (Radhiya Allaahu ´anhum); Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Hali ikishakuwa ndio hii na uhalisia wa mambo ndio huu ya kwamba miaka miatatu yote ilipita na hakukuwepo kitu cha aina hiyo, basi ni vipi watu wafanye kitu ambacho hakikufanywa na Maswahabah, Taabi´uun wala waliokuja nyuma ya Taabi´uun. Hii ni dalili tosha inayothibitisha kwamba hichi ni kitendo ambacho si sahihi na kwamba lau ingelikuwa kheri basi wangelitangulia Maswahabah wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Kwa sababu ndio wenye kutangulia katika kila kheri na wenye kupupia kila kheri.

Maulidi yalizuliwa katika karne ya nne. Kabla ya hapo hakukuwepo kitu kinachoitwa ´maulidi`. Yalizuliwa na kuvumbuliwa katika kane ya nne ya Hijriyyah. Walioyazua ni ´Ubaydiyyuun waliokuwa wanatawala Misri. Walizusha Bid´ah nyingi ikiwemo hii ya maulidi. Hayo yametajwa na al-Maqriyziy katika kitabu “al-Khutwatw wal-Aathaar” kuhusu tarehe ya Misri ambapo amesema kwamba walizusha maulidi sita:

1- Maulidi ya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

2- Maulidi ya Faatwimah (Radhiya Allaahu ´anhaa).

3- Maulidi ya ´Aliy (Radhiya Allaahu ´anh).

4- Maulidi al-Hasan (Radhiya Allaahu ´anh).

5- Maulidi ya al-Husayn (Radhiya Allaahu ´anh).

6- Maulidi ya kiongozi aliyekuweko miongoni mwa viongozi wao.

Kwa hivyo ni kitu kilichozuka katika karne ya nne ya Hijriyyah. Walioyazusha ni Raafidhwah ´Ubaydiyyuun. Walitegemea nini wakati wa kuyazusha? Kwa ajili ya kuwaigiza manaswara. Waliona ni vipi wao wasisherehekei kuzaliwa kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) ilihali manaswara wanasherehekea kuzaliwa kwa ´Iysaa? Kwa ajili hiyo ndio maana wakazusha jambo hili ambalo halina msingi wowote katika dini.

  • Mhusika: ´Allaamah ´Abdul-Muhsin bin Hamad al-´Abbaad
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: http://www.ajurry.com/vb/showthread.php?t=36078
  • Imechapishwa: 02/11/2019