Enyi ndugu! Dalili za wanaosema asiyeswali ni kafiri zina nguvu sana kabisa. Hivyo swalah isichukuliwe sahali. Kwa ajili hii Ahl-ul-Hadiyth wengi wakiwafuata Maswahabah wanaonelea kuwa asiyeswali ni kafiri. Miongoni mwao ni Ayyuub as-Sikhtiyaaniy, Ishaaq bin Raahuyah, Ahmad bin Hanbal kutokana na maoni yake (Rahimahu Allaah).

Upande mwingine kuna wanachuoni ambao wana dalili ambazo wanazitegemea ambazo wanaonelea asiyeswali sio kafiri. Isipokuwa tu yule anayehalalisha kuiacha, huyo wanamkufurisha. Wote ni katika Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah. Hatuwatukani hawa wala wale – Allaah awawie radhi wote – kwa kuwa ni maimamu, wenye kufanya Ijtihaad na Ikhlaasw, wanasihiaji na walio mbali na matamanio ya Khawaarij ambao wanakufurisha kwa madhambi na vilevile matamanio ya Murji-ah ambao wanazembea katika Uislamu. Wote wanafuata mfumo wa Allaah ya haki na ni wenye kutofautiana katika Ijtihaad zao.

Wenye kuonelea kuwa mwenye kuacha swalah ni kafiri – hata kama hii ndio kauli yenye dalili na yenye nguvu – ni katika maimamu wetu na viongozi katika hawa ni Maswahabah. Wenye kuonelea kuwa sio kafiri, ni kutokana na Ijtihaad zao kutoka katika baadhi ya maandiko. Huyu vilevile ni katika maimamu wetu na viongozi wetu. Kadhalika tunawanyanyua juu ya vichwa vyetu.

Hatusema kuwa ni Murji-ah kama wanavosema wapumbavu ambao wanafuata madhehebu ya Khawaarij. Kwa kuwa wanapomhukumu yule asiyemkufurisha mwenye kuacha swalah kwamba ni Murjiy´, wamewahukumu maimamu miongoni mwa maimamu wakubwa wa Uislamu, bali wanachuoni wengi wa Uislamu ilihali ni wenye kufanya Ijtihaad. Wanachokusudia kwa hukumu hizi ni kuilenga haki na hawafuati matamanio yao na sio wenye kutuhumiwa katika dini zao – Allaah awawie radhi wote.

  • Mhusika: ´Allaamah Rabiy´ bin Haadiy al-Madkhaliy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: adh-Dhariy´ah ilaa Bayaan Maqaaswid Kitaab-ish-Sharï´ah (1/517-518)
  • Imechapishwa: 26/08/2020