Swali: Ni ipi hukumu ya swalah? Ni ipi hukumu ya ambaye anachukulia wepesi kuswali mkusanyiko msikitini na badala yake anaswali peke yake? Ni ipi hukumu ya ambaye anachelewesha swalah mpaka nje ya wakati wake?

Jibu: Hapa kuna mambo matatu:

1 – Kuacha kuswali ni ukafiri unaomtoa mtu katika dini. Ikiwa yuko na mke, basi mke atatengana naye. Si halali kichinjwa chake. Haikubaliwi swawm wala swadaqah yake. Haijuzu kwake kuingia Haram ya Makkah. Akifa haijuzu kumswalia wala kumvisha sanda. Aidha hatoswaliwa swalah ya jeneza. Wala hatozikwa kwneye makaburi ya waislamu. Mambo yalivyo ni kwamba atatolewa nchi kavu na kuchimbiwa shimo na kutupwa ndani yake. Ambaye anafiwa na ndugu yake na yeye anajua kuwa haswali, si halali kwake akawadanganya watu na akawaacha wamswalie. Kwa sababu ni haramu kumswalia kafiri. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تُصَلِّ عَلَىٰ أَحَدٍ مِّنْهُم مَّاتَ أَبَدًا وَلَا تَقُمْ عَلَىٰ قَبْرِهِ ۖ إِنَّهُمْ كَفَرُوا بِاللَّـهِ وَرَسُولِهِ وَمَاتُوا وَهُمْ فَاسِقُونَ

”Wala kamwe usimswalie yeyote miongoni mwao akifa na wala usisimame kaburini kwake [kwa ajili ya kumuombea]; kwani hakika wao wamemkanusha Allaah na Mtume Wake na wakafa hali wao ni mafasiki.”[1]

مَا كَانَ لِلنَّبِيِّ وَالَّذِينَ آمَنُوا أَن يَسْتَغْفِرُوا لِلْمُشْرِكِينَ وَلَوْ كَانُوا أُولِي قُرْبَىٰ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمْ أَنَّهُمْ أَصْحَابُ الْجَحِيمِ

“Haimpasi Nabii na wale walioamini kuwaombea msamaha washirikina, japokuwa ni jamaa zao wa karibu, baada ya kuwabainikia kwamba wao ni watu wa Motoni.”[2]

2 – Ambaye haswali na mkusanyiko na badala yake anaswali nyumbani kwake ni mtenda dhambi nzito na si kafiri. Lakini akiendelea kufanya hivo anajumuishwa katika mafusaki na anaondokewa na sifa ya uadilifu.

3 – Ambaye anaichelewesha mpaka nje ya wakati wake dhambi yake ni mbaya zaidi kuliko ambaye haswali pamoja na mkusanyiko. Ni haramu na haijuzu kuchelewesha swalah mpaka ukatoka wakati wake pasi na udhuru unaokubalika kwa mujibu wa Shari´ah. Isitoshe swalah kama hiyo haisihi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote atakayefanya kitendo kisichokuwa ndani yake amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[3]

Swalah ni jambo muhimu sana. Ni lazima kwa muislamu kulitilia umuhimu. Swalah ndio nguzo ya Uislamu, kama kama alivosema Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Nyumba haiwezi kusimama kabisa bila ya nguzo. Kwa hivyo ni lazima kwa waislamu kunasihiana baina yao, kuamrishana nayo na waitilie bidii.

[1] 9:84

[2] 9:113

[3] Muslim (1718).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/35-36)
  • Imechapishwa: 07/04/2026