Ni namna gani muislamu anatakiwa kujiandaa kwa ajili ya Hajj na ´Umrah?

Swali 7: Vipi anajiandaa muislamu kwa ajili ya Hajj na ´Umrah?

Jibu: Kinachopasa kwa nuislamu kujiandaa nacho katika Hajj yake na ´Umrah yake ni kwamba ajitayarishe kwa kila ambalo linawezekana kwamba atalihitaji katika safari yake, katika mali, nguo, vifaa na vinginevyo. Kwa sababu huenda atalihitaji hilo katika nafsi yake au atalihitaji mmoja katika marafiki zake. Aidha ajitayarishe vilevile kwa kumcha Allaah, ambako maana yake ni kuchukua kinga dhidi ya adhabu ya Allaah kwa kufanya amri za Allaah na kujiepusha na makatazo Yake. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَتَزَوَّدُوا فَإِنَّ خَيْرَ الزَّادِ التَّقْوَىٰ ۚ وَاتَّقُونِ يَا أُولِي الْأَلْبَابِ

”Chukueni masurufu, hakika bora ya masurufu ni kumcha Allaah. Nicheni Mimi, enyi wenye akili![1]

Kumcha Allaah ni maandalizi ya kimaana ambapo mtu anajiandaa katika undani wa nafsi yake kwa ajili ya kukutana na Allaah (Ta´ala) na siku ya Mwisho. Matokeo yake anahakikisha kwamba anasimamisha yale ambayo Allaah amewajibisha juu yake na anaacha yale ambayo Allaah amemuharamishia.

Mara nyingi mno tunakutana na haja katika safari ambapo mtu anahitaji vitu ambavyo anadhani ni vyepesi basi havichukui pamoja navyo katika safari yake. Kisha ghafla anavihitaji au anavihitaji mmoja katikam marafiki zake. Kwa hiyo mtu we mwenye uthabiti, mwenye ujasiri na aliyejiandaa kwa yale anayotarajia kwamba yatakuwa hata kama yako mbali.

[1] 02:197

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (21/388)
  • Imechapishwa: 27/05/2026