Swali: Ni ipi hukumu ya kula mnyama ya nungunungu?

Jibu: Wanazuoni (Rahimahumu Allaah) wametofautiana kuhusu hukumu yake. Wapo walioihalalisha na wapo walioiharamisha. Sahihi ya maneno mawili ni kwamba ni halali, kwa sababu msingi katika wanyama ni uhalali na wala hauharamishwi miongoni mwao isipokuwa ule uliouharamishwa na Shari´ah. Haikupokelewa katika Shari´ah jambo linalofahamisha kuharamishwa kwa mnyama huyu. Naye hula mimea kama sungura na paa, wala si katika wanyama wakali wenye meno ya kushambulia. Hivyo hakuna sababu ya kumharamisha. Mnyama aliyetajwa ni aina ya vinyamkera na ngozi yake ina miiba mirefu. Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) kuhusu kinyamkera ambapo akasoma maneno Yake (Ta´ala):

قُل لَّا أَجِدُ فِي مَا أُوحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَىٰ طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلَّا أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ

“Sema: “Sipati katika yale niliyofunuliwa Wahy kwangu kilichoharamishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu [mzoga] au damu inayomwagika au nyama ya nguruwe – kwani hiyo ni uchafu.”[1]

Kisha mzee aliyekuwa naye akasema: ”Hakika Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ´anh) amepokea kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba amesema:

“Hakika huyo ni mchafu katika wachafu.”

Ibn ´Umar (Radhiya Allaahu ´anhumaa) akasema: ”Ikiwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema hivo, basi ni kama alivyosema.”[2]

Hivyo imebainika katika maneno yake (Radhiya Allaahu ´anh) kwamba hakujua kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema chochote kuhusu kinyamkera. Pia imebainika katika maneno yake kwamba hakumthibitishia mzee huyo.

Hadiyth iliyotajwa imedhoofishwa na al-Bayhaqiy na wengine miongoni mwa wanazuoni kwa sababu ya kutokujulikana kwa mzee huyo. Kwa hiyo imejulikana kutokana na tuliyotaja usahihi wa maoni ya kuhalalisha na udhaifu wa maoni ya kuharamisha. Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) ndiye mjuzi zaidi.

[1] 6:145

[2] Ahmad (8597).

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (23/35-36)
  • Imechapishwa: 22/02/2026