Mwanamke kunyoa nywele za sehemu za siri baada ya kila hedhi

Swali 5007: Je, mwanamke analazimika kunyoa nywele za sehemu za siri baada ya kila hedhi?

Jibu: Kuondoa nywele za sehemu za siri kwa kuzinyonyoa, kutumia dawa ya kuondoa nywele, kunyoa au kukata ni miongoni mwa Sunnah za kimaumbile ambazo Uislamu umehimiza na kuzipendekeza. Lakini Uislamu haujaweka muda huo kuwa ni baada ya kila hedhi. Ahmad, al-Bukhaariy, Muslim na watunzi wa vitabu vya Sunan wamepokea ya kwamba Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Mambo matano ni katika maumbile: tohara, kunyoa nywele za sehemu za siri, kupunguza masharubu, kukata kucha na kung’oa nywele za kwapani.”[1]

Imesihi pia kwamba Anas (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Tuliwekewa muda wa kupunguza masharubu, kukata kucha, kung’oa nywele za kwapani na kunyoa nywele za sehemu za siri, kwamba tusiziachie zaidi ya usiku arobaini.”[2]

Ameipokea Muslim na Ibn Maajah. Ahmad, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Abu Daawuud wameipokea kwa tamko lisemalo:

“Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alituwekea muda…”

[1] Ahmad (02/229), al-Bukhaariy (07/56) na Muslim (01/153) na wengineo.

[2] Muslim (153), Abu Daawuud (4200) na wengineo.

  • Muhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (5/127-128)
  • Imechapishwa: 21/10/2026