Swali:  Wanawake siku ya ijumaa wanaswali swalah za Sunnah na wakisema kuwa hiyo ni Sunnah ya ijumaa saa fulani ambapo wanaswali Rak´ah nne au mbili kabla ya swalah…

Jibu: Wanawake hawawajibiki kuswali ijumaa na wala hawana Sunnah ya ijumaa. Ijumaa ni kwa wanaume na haina Sunnah kabla yake. Sunnah yake ni baada yake ambazo ni Rak´ah mbili au nne, ni mamoja iwe msikitini au nyumbani. Ama kabla ya ijumaa, mtu huswali yale aliyomjaalia Allaah kama ni Rak´ah mbili, nne, sita, nane au zaidi. Hakuna idadi maalum. Hakuna Raatibah maalum kabla yake. Lakini mtu huswali siku ya ijumaa yale yanayomwepesia kabla ya swalah na baada yake huswali Rak´ah mbili au nne. Imethibiti kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiswali Rak´ah mbili nyumbani kwake. Amesema (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mwenye kuswali baada ya ijumaa, basi aswali nne.”

Akiswali nne ni bora zaidi na akiswali mbili inatosha.

Ama wanawake hawawajibiki kuswali ijumaa wanaposwali majumbani mwao. Wakiswali Dhuhaa hiyo ni swalah ya Dhujaa, si swalah ya ijumaa. Wakiswali majumbani mwao Dhuhaa siku ya ijumaa, hiyo huitwa ”Swalah ya Dhuhaa”, si Sunnah ya ijumaa. Ama wakiswali pamoja na watu msikitini, basi wanaswali pamoja na watu kama wanavyoswali wengine: Rak´ah mbili za ijumaa na hiyo inawatosheleza badala ya Dhuhr. Ikiwa mwanamke ataswali pamoja na watu msikitini siku ya ijumaa, basi inamtosheleza badala ya Dhuhr. Akiswali kabla yake Rak´ah kadhaa, hiyo ni Sunnah ya Dhuhaa na si Sunnah ya ijumaa. Akiswali baada yake, basi huswali Rak´ah mbili au nne kama Sunnah ya ijumaa ikiwa aliswali pamoja na watu. Ama akiwa nyumbani, hana Ijumaa. Badala yake ataswali Dhuhr Rak´ah nne nyumbani kwake. Hana swalah ya ijumaa nyumbani. Akiswali pamoja na watu, basi ataswali pamoja nao Rak´ah mbili na itamtosheleza.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3346/حكم-سنة-الجمعة-القبلية-والبعدية
  • Imechapishwa: 29/09/2026