Swali: Ni ipi hukumu ya mwanamke kuswali na nguo za wanaume?

Jibu: Ikiwa nguo hiyo anayovaa ni maalum kuvaliwa na wanaume, basi kuile kuivaa kwake ni haramu, ni mamoja wakati wa kuswali na nje ya swalah. Ibn ´Abbaas (Radhiya Allaahu ´anhumaa) amesema:

”Allaah amewalaani wanawake wenye kujifananisha na wanaume na wanaume wenye kujifananisha na wanawake.”[1]

Kwa hivyo si halali kwa mwanamke kuvaa nguo ambayo ni maalum kwa wanaume, na si halali kwa mwanaume kuvaa nguo ambayo ni maalum kwa mwanamke.

Lakini tunapaswa kujua ni kipi kinchoamua kuwa nguo ni ya jinsia fulani au sio ya jinsia fulani. Haihusiani na rangi peke yake, bali inahusiana na rangi na sifa. Kwa ajili hiyo inafaa kwa mwanamke kuvaa nguo nyeupe ikiwa mshono wake sio kama nguo za wanaume.

Ikishathibiti kuwa ni haramu kwa mwanamke kuvaa nguo ambayo ni maalum kwa wanaume, basi ni haramu kuswali ndani yake. Baadhi ya wanazuoni wanashurutisha kwamba ni lazima kile chenye kumfunika kiwe cha halali. Wanazuoni wamekinzana juu ya jambo hilo. Baadhi ya wanazuoni wameshurutisha kwamba ni lazima kwa kile chenye kufunika kiwe cha halali, wengine hawakushurutisha jambo hilo.

Wale wanaoshurutisha jambo hilo wanajengea hoja kwamba kufunika uchi ni moja miongoni mwa sharti za swalah, na kwamba ni lazima sharti iwe miongoni mwa vile ambavyo Allaah ameviidhinisha; ikiwa Allaah hakuvitolea idhini basi hakihesabiki kuwa ni chenye kufunika kwa mujibu wa Shari´ah.

Wale wasioshurutisha jambo hilo wanasema kuwa swalah inasihi ingawa mtu anapata dhambi. Hoja yao ni kwamba ufunikaji umetekelezwa na dhambi ni yenye kutoka nje ya ufunikaji na haikufupika na swalah, kwa sababu imeharamishwa kuvaa nguo ya haramu ndani na nje ya swalah.

Kwa hali yoyote ile, kuna khatari ya kutokukubaliwa swalah yake kwa yule mwenye kuvaa nguo ya haramu.

[1] al-Bukhaariy (10/274), Abu Daawuud (2/305), ad-Daarimiy (2/280-281) na Ahmad (1982) kupitia kwa Hishaam ad-Dastawaa-iy, kutoka kwa Yahyaa bin Abiy Kathiyr, kutoka kwa ´Ikrimah, kutoka kwa Ibn ´Abbaas.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/301-302)
  • Imechapishwa: 11/06/2026