Mswaliji anahisi kutokwa na kitu ndani ya swalah yake

Swali: Mara nyingi baada ya wudhuu´ au wakati wa swalah nahisi kana kwamba tone linatoka kwenye dhakari yangu. Lakini sijui ikiwa ni mkojo au kitu kingine. Je, swalah na wudhuu´ wangu vinakuwa batili kwa kuhisi hivyo tu? Je, nitoke katika swalah na nirudie swalah au nisiache?

Jibu: Ikiwa hali ni kama ulivyoeleza, usitoke ndani ya swalah yako kwa sababu hiyo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alipolalamikiwa kuhusu mtu anayehisi kitu wakati wa swalah, akasema:

“… asiondoke msikitini mpaka asikie sauti au ahisi harufu.”[1]

Kuna maafikiano juu ya usahihi wake.

Pia kwa sababu hayo yanatokana na shaytwaan ambaye anataka kuharibu swalah na wudhuu´ wako. Kwa hiyo usiyape umuhimu mpaka ujue kwa yakini kwamba kuna kitu kimetoka kwako, kama ilivyojulisha Hadiyth iliyotajwa hapo juu. Ikiwa utajua kwamba kuna kitu kimetoka kwako wakati wa swalah, basi ni wajibu kwako kurudia wudhuu´ na swalah, ni mamoja uwe imamu, unaswali peke yako au ni maamuma.

[1] Muslim (01/190).

  • Muhusika: al-Lajnah ad-Daaimah
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Fataawaa al-Lajnah ad-Daaimah (5/279-280)
  • Imechapishwa: 09/11/2026