Mkusanyiko unaswali kinyume na Qiblah

Swali: Ni ipi hukumu mkusanyiko ukiswali swalah kinyume na Qiblah?

Jibu: Swali hili limegawanyika katika hali mbili:

1 – Wawepo maeneo ambayo hawawezi kujua ni wapi kipo Qiblah, kwa mfano wapo safarini na mbingu ikawa na mawingu. Katika hali kama hiyo wakajitahidi na baadaye ikabainika kuwa wameswali kinyume na Qiblah, hakuna chochote kinachowalazimu. Kwa sababu wamemcha Allaah wawezavyo. Allaah (Ta´ala) amesema:

فَاتَّقُوا اللَّـهَ مَا اسْتَطَعْتُمْ

”Mcheni Allaah muwezavyo.”[1]

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Ninayokukatazeni basi jiepusheni nayo na nikikuamrisheni jambo basi lifanyeni muwezavyo.”[2]

Isitoshe Allaah (Ta´ala) amesema kuhusiana na suala hili:

وَلِلَّـهِ الْمَشْرِقُ وَالْمَغْرِبُ ۚ فَأَيْنَمَا تُوَلُّوا فَثَمَّ وَجْهُ اللَّـهِ ۚ إِنَّ اللَّـهَ وَاسِعٌ عَلِيمٌ

”Mashariki na Magharibi ni milki ya Allaah. Hivyo basi, popote mnapogeuka kuna uso wa Allaah. Hakika Allaah ni Mwenye wasaa, Mjuzi wa yote.[3]

2 – Wakawepo maeneo ambapo wanaweza kukiuliza Qiblah kilipo lakini hata hivyo wakazembea na kupuuza. Katika hali kama hii wanalazimika kuzilipa swalah walizoswali kinyume na Qiblah, ni mamoja wamejua kuwa wamesali kimakosa kabla kumalizika kwa muda wa swalah au baada yake. Kwa sababu katika hali hii wamekosea na wametenda dhambi. Wamekosea kwa kuswali kinyume na Qiblah, kwa sababu hawakukusudia kupinda kutokana nach, lakini wametenda dhambi kwa sababu ya kupuuza na kutouliza kwao. Hata hivyo inatakiwa itambulike kuwa upindaji mdogo wa Qiblah haudhuru, kwa mfano mtu akapinda kiasi kidogo upande wa mashariki au wa magharibi. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema kuhusu wakazi wa Madiynah:

“Baina ya mashariki na magharibi ni Qiblah.”[4]

Wale wanaoeshi upande wa kaskazini mwa Ka´bah tunawaambia kuwa baina ya mashariki na magharibi ni Qiblah. Kadhalika wanaoeshi upande wa kusini mwake na wale wanaoeshi upande wa mashariki au upande wa magharibi tunawaambia kuwa baina ya kaskazini na kusini ni Qiblah. Upindaji mdogo hauathiri na wala haudhuru. Napenda kuzindua jambo moja: Wale walioko katika msikiti Mtakatifu na wanaiona Ka´bah basi wanalazimika kuielekea yenyewe, na si kuelekea tu upande wake, wanaposwali. Kwa sababu wakipinda kutokana na Ka´bah hawawi ni wenye kukielekea Qiblah. Nawaona watu wengi katika msikiti Mtakatifu hawaielekei Ka´bah yenyewe. Utaona safu ndefu ya mviringo na hapo ndipo utajua vyema kuwa wengi wao hawakuswali kwa kuielekea Ka´bah yenyewe. Hili ni kosa kubwa ambalo waislamu wanapaswa kuzinduka nalo. Wakiswali katika hali hii, basi wameswali kwa kutokielekea Qiblah.

[1] 64:16

[2] al-Bukhaariy (7288) na Muslim (1337).

[3] 2:115

[4] at-Tirmidhiy (342) na Ibn Maajah (1011). al-Haakim ameisahihisha katika ”al-Mustadrak” (1/255) adh-Dhahabiy akaafikiana naye.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/415-416)
  • Imechapishwa: 02/04/2026