Masharti ya ´Aqiyqah, wakati wake na sifa zake

Swali: Ni nini ´Aqiyqah? Ni yepi masharti yake, sifa zake ni zipi na ni wakati gani hufanywa? Je, inajuzu kuigawa mafungu matatu kama Udhhiyah au kuifanya ni karamu na kuwaalika jamaa?

Jibu: ´Aqiyqah pia huitwa ”an-Nasiykah”. Baadhi ya watu huiita ”at-Tamiym”. Nayo ni mnyama anayechinjwa kwa ajili ya mtoto katika siku ya saba. Nayo ni kama Udhhiyah, kwa maana umri wake ni kama wa Udhhiyah: kondoo wa kufikia umri unaokubalika au mbuzi aliyefikia umri unaokubalika. Kwa mtoto wa kiume huchinjwa wawili na kwa mtoto wa kike mmoja. Bora zaidi ni siku ya saba, lakini akichinja baada ya hapo inajuzu, ingawa siku ya saba ni bora zaidi.

Mtu anayo khiyari; akitaka anaweza kuigawa kwa masikini, majirani na jamaa, akitaka anaweza kuifanya ni karamu na kuwaalika anaowataka katika jamaa na majirani zake na akitaka anaweza kugawa sehemu yake na kula sehemu nyingine pamoja na ndugu na majirani zake. Inapendekezwa kuwapa masikini sehemu kadiri itakavyowezekana.

Swali: Je, inajuzu mjomba kumfanyia ´Aqiyqah au ni lazima baba ndiye afanye?

Jibu: Bora zaidi ni baba na yeye ndiye anayewajibika kwanza. Lakini akifanya mwingine badala yake, hakuna ubaya. Ikiwa mama, ndugu, mjomba au ami atamfanyia, inatosha.

Swali: Vipi uwakala unasihi?

Jibu: Ndio, uwakala unasihi.

Swali: Vipi mapacha?

Jibu: Mapacha pia ni hivyo hivyo. Kila mtoto ana hukumu yake. Ikiwa wote ni wavulana wawili, basi kila mmoja anachinjiwa wawili. Ikiwa ni mvulana na msichana, basi watatu ambapo wawili kwa mvulana na mmoja kwa msichana. Ikiwa wote ni wasichana wawili, basi kila mmoja anachinjiwa mnyama mmoja.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3283/شروط-العقيقة-ووقتها-وصفاتها
  • Imechapishwa: 10/10/2026