Swali: Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala) amesema:

وَقُلِ اعْمَلُوا فَسَيَرَى اللَّـهُ عَمَلَكُمْ وَرَسُولُهُ وَالْمُؤْمِنُونَ

”Na sema [uwaambie]: ”Fanyeni [mtakavyo]. Allaah ataona matendo yenu na Mtume Wake na waumini.”[1]

Je, maiti anawajua na kuonyeshwa matendo ya familia yake? Je, huwajua wanapomtembelea?

Jibu: Maiti kuijua familia yake na kujua matembezi ya wanaomtembelea ni jambo linalotakiwa kutazamwa vyema. Hakuna dalili ya wazi juu ya hilo. Maana ya Aayah – Allaah ndiye anajua zaidi – ni kwamba Allaah huwaona watu siku zote. Yeye anayaona matendo yao. Waumini wanayaona matendo yao hapa duniani. Siku ya Qiyaamah matendo yatawekwa wazi mbele ya watu. Vivyo hivyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akiyaona matendo ya watu katika uhai wake hapa duniani na pia atayaona siku ya Qiyaamah pale yatakapowekwa wazi mbele ya mashahidi wote.

Katika maana hii kuna kuhimiza kufanya matendo mema na kwamba yatafunuliwa. Waumini wanaona mema ya mtu hapa duniani, Allaah anayaona, waumini watayaona siku ya Qiyaamah na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) atawaona siku ya Qiyaamah na alikuwa anayayaona katika uhai wake miongoni mwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Hivyo kuna kuhimiza kufanya mema na kuyaonyesha, kwa sababu jambo hilo linampa heshima mtu, humfanya atende mema na ajitahidi katika mambo ya kheri. Kwa kuwa mema hayo yataonekana na waumini duniani, atasifiwa kwayo na atapata kutajwa kwa maneno mazuri miongoni mwa watu. Aakhirah yatawekwa wazi mbele ya watu na kusemwa: haya ni matendo ya fulani. Atasemewa hadharani na mizani yake itakuwa nzito na atapata kheri kubwa siku ya Qiyaamah. Kinyume chake ni kinyume chake. Tunamuomba Allaah atupe salama.

[1] 09:105

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1008/حقيقة-معرفة-الميت-اهله-وعرض-اعمالهم-عليه
  • Imechapishwa: 07/01/2026