Lini anafunga ambaye hakuweza kuchinja Hadiy katika Tamattu´?

Swali: Ni lini huanza kufunga yule ambaye hakuweza kuchinja Hadiy katika hajj ya Tamattu´?

Jibu: Anapomaliza ´Umrah yake huanza kufunga, hata kama ni katika Dhul-Qa´dah au Shawwaal. Atafunga siku tatu. Zile siku saba inapendekezwa azicheleweshe mpaka arudi katika nchi yake. Lakini akizifunga Makkah hakuna tatizo, kwa kuwa Allaah amesema:

فَمَن لَّمْ يَجِدْ فَصِيَامُ ثَلَاثَةِ أَيَّامٍ فِي الْحَجِّ وَسَبْعَةٍ إِذَا رَجَعْتُمْ ۗ تِلْكَ عَشَرَةٌ كَامِلَةٌ

”Asiyepata afunge siku tatu katika hajj na saba mtakaporejea – hizo ni kumi kamili.”[1]

Ni bora afunge zile tatu kabla ya ´Arafah ili siku ya ´Arafah awe mwenye kula. Ikiwa hakupata nafasi kabla ya ´Arafah kwa sababu alikuwa na matumaini ya kununua kichinjwa cha Hadiy kisha akashindwa, basi atafunga siku za Tashriyq. Hii ni ruhusa maalum kwa yule aliyeshindwa kuchinjwa na hakupata fursa ya kufunga kabla ya ´Arafah. Atafunga siku za Tashriyq pekee pasina watu wengine, kwani hizo ni siku za kula, kunywa, kumtaja Allaah na kuchinja. Kwa hiyo haijuzu kuzifunga kwa mtu yeyote isipokuwa kwa yule aliyeshindwa kuchinja Hadiy na hakuweza kufunga kabla ya ´Arafah.

[1] 02:196

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/29417/متى-يصوم-من-لم-يستطع-الهدي-في-التمتع
  • Imechapishwa: 10/08/2025