Kumpa mtoto mmoja zawadi pasina wengine

Swali: Ikiwa mtu ameacha watoto wake wote wakiwa wakubwa na wameshaingia ndani ya ndoa. Miongoni mwao kuna msichana mnyonge, kisha akausia kuwa apewe sehemu ya mali yake zaidi ya urithi, kwa mfano apewe kitu cha ziada ili aolewe au kwa sababu ni mwanamke dhaifu.

Jibu: Hapana, si sahihi kumtenga mtoto yeyote kwa kumpa zaidi ya wengine. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Mcheni Allaah na fanyeni uadilifu baina ya watoto wenu.”

Hakuruhusu kumtenga mmoja kwa kitu maalum. Kwa hiyo hairuhusiwi kuusia kwa msichana au wengine zaidi ya urithi waliopangiwa na Shari´ah. Hata kama watoto wengine ni wakubwa, wameshaingia ndani ya ndoa, wana kazi, na kuna wadogo au dhaif, haijuzu kuwabagua kwa kuwapa chochote cha ziada katika wasia. Riziki yao iko mikononi mwa Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala). Urithi uwe sawa baina yao wote, ni mamoja awe mtu tajiri anayemiliki mamilioni au awe dhaifu asiyejiweza. Wanagawana kwa mujibu wa mgawanyo uliowekwa na Allaah (Ta´ala). Kwa hivyo haijuzu kumpa mnyonge chochote cha ziada kupitia wasia. Huo ndio msimamo sahihi wa wanazuoni. Hilo ni kutokana na maneno yake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam):

“Mcheni Allaah na fanyeni uadilifu baina ya watoto wenu.”

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1127/حكم-اعطاء-احد-الاولاد-دون-غيره
  • Imechapishwa: 30/01/2026