Kufukua kaburi kwa ajili ya kumzika maiti mwengine

Swali: Miji katika nyakati za karibuni imeona msongamano katika ujenzi na wakazi wake, jambo ambalo limejumuisha hata makaburi ya waislamu. Imeshuhudiwa kuwa kaburi hufunguliwa baada ya miezi minane tangu kuzikwa kwa maiti ndani na hukusanywa mabaki ya maiti, kisha huwekwa maiti mwingine. Je, una maoni gani juu ya hilo na khaswa ikiwa matendo ya wale wanaozikwa ndani ya kaburi yanatofautiana: miongoni mwao wako wenye matendo mema na miongoni mwao wasiokuwa hivo?

Jibu: Baraza la wanazuoni wakubwa limejadili suala hili mara kadhaa na likaamua kwamba ni wajibu yatengwe makaburi yatakayoenea watu, khaswa katika kisiwa na nchi zilizomo ndani ya kisiwa, kwa sababu humo kuna ardhi nyingi na magari yapo. Kwa hiyo ni lazima itengwe ardhi kubwa itakayoenea watu na kila kaburi liwe peke yake, kama alivyofanya Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah Madiynah, Makkah na sehemu nyinginezo. Kila mtu azikwe kaburini peke yake, isipokuwa ikitokea maafa au msiba mkubwa na wafu wakawa wengi, katika hali hiyo hapana neno wawili au watatu wakakusanywa kaburini pamoja kwa dharurah na kwa haja. Hivyo ndivo ilivyokuwa siku ya Uhud walipokuwa maiti ni wengi na waislamu walikuwa na majeraha na wakiogopa shari ya adui. Kwa sababu hiyo waliwazika wawili au watatu katika kaburi moja. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alikuwa akimtanguliza mbora wao upande wa Qiblah. Ama ikiwa watu wako katika amani na afya, basi ni wajibu kila mmoja azikwe kaburini peke yake na asizikwe pamoja na mwingine. Ardhi zipo. Iwapo mambo yatazidi kuwa magumu na wakiwa katika nchi yenye upungufu wa ardhi na isipatikane ardhi ya kutosha, basi inajuzu kwao kuwazika makundi. Lakini kwa kawaida katika nchi nyingi ardhi ipo. Wakitoka kidogo tu nje ya mji watapata ardhi wanayoweza kumzika kila mmoja peke yake na kumpeleka kwa magari, treni, magari ya kubebea mizigo na mengineyo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/30065/ما-حكم-فتح-القبر-لوضع-ميت-اخر-فيه
  • Imechapishwa: 08/09/2025