Swali: Mwanamke anachelewesha swalah ya Maghrib mwanzoni mwa wakati wake kwa sababu ya kusikiliza kipindi cha redio cha “Nuur ´alaad-Darb”. Je, anapata dhambi kwa ucheleweshaji huu pamoja na kuzingati kwamba anaiswali kabla ya kutoka wakati wake?

Jibu: Hapati dhambi kwa ucheleweshaji huu muda wa kuwa anaiswali swalah kabla ya kumalizika wakati wake. Kama inavyotambulika wakati wa Maghrib unaenda mpaka kuingia kwa ´Ishaa, bi maana takriban dakika 75 au mfano kama huo kuanzia kuzama kwa jua. Wakati mwingine baina yake kunakuwa na dakika 90. Muhimu ni kutambua kuwa hapana vibaya kuchelewesha Maghrib kwa ajili ya kusikiliza kipindi cha redio cha “Nuur ´alaad-Darb”. Kipindi kama hicho na vipindi vingine vya kidini ni vya kielimu. Hakuna yeyote asiyejua fadhilah za kuwa na elimu na kuitafuta. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Yeyote mwenye kushika njia akitafuta kwayo elimu, basi Allaah humfanyia wepesi njia ya kuelekea Peponi.”

Kutafuta elimu ni katika ´ibaadah bora kabisa. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hakuna chochote kinacholingana na elimu kwa ambaye itakuwa njema nia yake.” Wakasema: “Ni vipi nia inafanywa kuwa njema, ee Abu ´Abdillaah?” Akajibu: “Anuie kujiondoshea ujinga mwenyewe na kutoka kwa wengine.”

Lau Allaah atajua nia ya mwanamke huyu msikilizaji kwamba kama isingelikuwa kwa sababu ya kusikiliza kipindi hichi cha redio basi angeswali mwanzoni mwa wakati wake, basi anamlipa thawabu kama aliyeswali mwanzoni mwa wakati. Kwa sababu amechelewesha swalah mwanzoni mwa wakati wake kutokana na manufaa kwa mujibu wa Shari´ah ambayo pengine yakawa ni bora zaidi kuliko kuitanguliza swalah mwanzoni mwa wakati wake.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/28-29)
  • Imechapishwa: 08/04/2026