Kuashiria kidole cha shahaadah kwa mikono yote miwili

Swali: Baadhi ya waswaliji huinua kidole cha shahaadah cha mikono yote miwili ya kushoto na ya kulia wakati wa Tashahhud. Baadhi yao huvaa miwani wakati wa swalah. Baadhi yao huweka kifaa cha simu ambacho mara nyingi hutoa sauti wakati wa swalah, jambo linalowashughulisha wanaoswali. Ni ipi hukumu ya matendo haya?

Jibu: Ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwa mwenye kuswali kuashiria kwa kidole cha shahaadah cha mkono wake wa kulia anapokaa katika Tashahhud ya kwanza na ya mwisho. Aidha inapendekezwa kukitikisa wakati wa kuomba du´aa katika Tashahhud ya mwisho. Anapaswa kukunja kidole kidogo na kidole kinachofuata, na kuunganisha kidole gumba pamoja na cha kati kwa mviringo na kuweka mkono wake juu ya paja lake la kulia. Ama mkono wa kushoto uwe juu ya paja lake la kushoto, akiwa amenyosha vidole vyake kuelekea goti.

Asiashirie kwa kidole cha shahaadah cha mkono wa kushoto, bali anakinyosha pamoja na vidole vingine. Kwa sababu jambo hilo halikupokelewa kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) katika tulichokijua katika Sunnah zake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Vilevile imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba alikuwa anakunja vidole vyake vyote vya mkono wa kulia isipokuwa kidole cha shahaadah katika Tashahhud ya kwanza na ya mwisho. Hivyo inapendekezwa kwa mwenye kuswali kufanya hivi wakati mwingine na vile wakati mwingine, kwa sababu yote mawili yamethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): kuunganisha gumba na kidole cha kati huku akikunja kidole kidogo na kinachofuata, na kuashiria kwa kidole cha shahaadah, au kukunja vidole vyote isipokuwa kidole cha shahaadah.

Aidha inapendekezwa kwa mwenye kuswali kuzima simu au kifaa cha kuita ili kisimsumbue yeye wala wengine. Inachukiza kwake kushughulika kuvaa miwani wakati wa swalah ikiwa hakuna haja ya kufanya hivyo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (29/300)
  • Imechapishwa: 08/03/2026