Je, inafaa kujifunza na kufundisha uchawi kwa lengo zuri?

Swali: Nakuambia, ee Shaykh ninakupenda kwa ajili ya Allaah, Allaah akuongezee umri katika utiifu Wake. Nimeangalia kitabu “Rawaa’iy´-ul-Bayaan” cha as-Swaabuniy na katika tafsiri ya maneno ya Allaah (Subhaanahu wa Ta´ala):

وَاتَّبَعُوا مَا تَتْلُو الشَّيَاطِينُ عَلَىٰ مُلْكِ سُلَيْمَانَ ۖ وَمَا كَفَرَ سُلَيْمَانُ

”Wakafuata yale waliyoyasoma mashaytwaan kuhusu ufalme wa Sulaymaan. Sulaymaan hakukufuru… “[1]

ambapo akasema kuwa uchawi uko aina mbili:

1 – Aliyejifunza ili ajilinde nao au kuzuia madhara yake kwa watu, basi ameokoka na amesimama juu ya imani.

2 – Aliyejifunza akiitakidi kuwa ni sahihi ili kuwadhuru watu, basi amepotea na amekufuru. Hivyo watu wakawa makundi mawili. Tunaomba ufafanuzi wa hilo.

Jibu: Kuhusu kusema kwako unanipenda kwa ajili ya Allaah, basi nasema kwamba Allaah akupende ambaye umetupenda kwa ajili Yake. Tunamuomba Allaah atufanye sisi na nyinyi miongoni mwa wanaopendana kwa ajili Yake. Imesihi kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah atasema siku ya Qiyaamah: “Wako wapi wanaopendana kwa ajili ya utukufu Wangu? Leo Nitawafunika kivulini Mwangu siku ambayo hakuna kivuli isipokuwa kivuli Changu.”

Tunamuomba Allaah atujalie tuwe miongoni mwao.

Ama kuhusu kitabu “Rawaa’iy´-ul-Bayaan” cha as-Swaabuniy sikukisoma. Lakini ikiwa ameruhusu ndani yake kujifunza uchawi, basi amekosea na amefanya kosa kubwa. Haijuzu kujifunza uchawi hata kama mtu ana nia njema. Kwa sababu kujifunza uchawi hakufanyiki isipokuwa kwa kumkufuru Allaah – tunajilinda kwa Allaah. Hakufanyiki isipokuwa kwa kuwaabudu mashaytwaan na kujikurubisha kwao ili wamfundishe yale wanayodai kuwa ni mambo ya ghaibu.

Kwa hiyo ninachotaka kusema ni kwamba kujifunza uchawi na kuwafundisha watu ni jambo la maovu, halijuzu kwa wanazuoni wa haki, ni mamoja awe amesema as-Swaabuniy au mtu mwingine, halijuzu kabisa. Bali ni jambo la maovu. Ikiwa amesema maneno hayo, basi amekosea vibaya sana.

[1] 02:102

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3148/تعلم-السحر-وتعليمه-للناس-منكر-لا-يجوز
  • Imechapishwa: 02/11/2026