´Ishaa ya msafiri nyuma ya imamu anayeswali Tarawiyh

Swali: Mtu ambaye ni msafiri aliingia msikitini kuswali swalah ya ´Ishaa na imamu alikuwa anaswali Tarawiyh. Akajiunga pamoja naye kwa nia ya swalah ya ´Ishaa kwa kufupisha swalah. Je kitendo chake hiki ni sahihi?

Jibu: Hakuna ubaya katika hilo. Kwa sababu imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kinachofahamisha kujuzu kwa anayeswali faradhi kuswali nyuma ya anayeswali swalah inayopendeza. Jengine ni kwa sababu swalah ya msafiri ni Rak´ah mbili na swalah ya Tarawiyh ni Rak´ah mbilimbili. Kwa maanaa nyingine ni kwamba hakuna tofauti katika idadi.

Ama kama msafiri ataswali nyuma ya mkazi anayeswali Dhuhr, ´Aswr au ´Ishaa, basi atalazimika kuswali Rak´ah nne hata kama hakumpata imamu isipokuwa sehemu ya swalah. Kwa sababu Sunnah imesihi kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kufanya namna hiyo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (30/166)
  • Imechapishwa: 07/03/2026