Imamu anampatia kazi yake mwingine kukaa nafasi yake

Swali: Naomba kutoka kwenu kubainisha hukumu ya Shari´ah kuhusu imamu wa msikiti kumteua mtu mwingine miongoni mwa maimamu au wahifadhi wa Qur-aan kuswali kwa niaba yake, huku yeye hahudhurii isipokuwa siku ya ijumaa kwa hoja kwamba ana shughuli nyingine ilihali anapokea mshahara wa kila mwezi na humpa sehemu yake anayekaa kwa niaba yake.

Jibu: Kinachodhihiri kwangu ni kwamba haijuzu kwa imamu huyu kufanya alivyotajwa na muulizaji isipokuwa kwa kurejea kwa chombo husika kinachosimamia jambo hilo. Aeleze kwa chombo hicho kuwa ana shughuli na hawezi kuhudhuria isipokuwa siku fulani au siku ya ijumaa. Iwapo watamkubalia na kumruhusu ateue wa kumkalia niaba, basi amteue anayemuona kuwa yuko sawa naye au bora zaidi yake katika kuswalisha, katika kusoma na katika elimu ili anayekaa kwa niaba yake awe anasimama mahali pake katika kila jambo. Ama imamu kupokea mshahara kisha akakabidhi kazi kwa mwingine, hilo halijuzu isipokuwa kwa idhini ya chombo husika. Wakimruhusu na wakamteua anayefaa kuwa naibu wake, basi hakuna ubaya katika hilo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (30/138)
  • Imechapishwa: 04/03/2026