Swali: Mlisema katika Khutbah ya ijumaa iliyopita kwamba swalah ya ijumaa inasimama kwa watu wasiopungua watatu. Lakini katika kitabu cha Fiqh cha kiwango cha msingi kimeeleza kwamba inashurutishwa kuwepo watu arobaini miongoni mwa wakazi waliobaleghe ili ijumaa iwe sahihi. Vipi tutakusanya kati ya maoni haya mawili, kwani tulipoulizwa na baadhi ya wanafunzi tulipata uzito kujibu?

Jibu: Sharti la watu arobaini ni maoni ya baadhi ya wanazuoni na hayo ndio maoni ya Hanbaliy ambayo ndiyo yanayofundishwa katika baadhi ya shule na yanajulikana kwa kikosi cha wanazuoni. Lakini maoni yaliyo sahihi zaidi ni kwamba haisurutishwi kuwepo watu arobaini na hakuna dalili sahihi inayothibitisha sharti hilo. Hadiyth inayotaja sharti la arobaini ni dhaifu. Hivyo ikiwa watu wa kijiji wamekusanyika – ni mamoja iwe ni kumi, ishirini au hata watano waliokaa kwa kudumu katika kijiji – basi imewekwa katika Shari´ah kwao kuswali ijumaa kama wanavyoswali swalah ya mkusanyiko na haisurutishwi kufikia arobaini kwa mujibu wa mujibu wa maoni sahihi ya wanazuoni. Ni kweli kwamba suala hili lina makinzano makubwa miongoni mwa wanazuoni. Lakini maoni yaliyo na nguvu zaidi ni haya; kwa kuwa hakuna dalili ya kuweka idadi maalum zaidi ya watatu. Watatu ndio kiwango cha chini kinachoweza kuitwa mkusanyiko: imamu mmoja na maamuma wawili na hapo swalah ya ijumaa inatekelezwa.

Swali: Je, kwa hali hiyo ijumaa inakuwa ni wajibu juu yao?

Jibu: Ndiyo.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3189/العدد-الذي-تقام-به-صلاة-الجمعة
  • Imechapishwa: 26/10/2026