Swali: Bila shaka kusema kuwa ni haramu kuigiza Maswahabah ni maoni yenye nguvu na pia waliokuja baada yao. Lakini, je, huoni kuwa kuigiza watu wengine wema kunaweza kubadilisha tabia za watu na kuwa ni njia ya kulingania kwa Allaah, khaswa ikiwa imethibitika kielimu kuwa ni jambo lina athari kwa watazamaji?

Jibu: Kuigiza hakujuzu, ee ndugu yangu. Kuigiza ni uongo na uzushi. Hakujuzu, si kwa Maswahabah wala kwa wasiokuwa Maswahabah. Kile kilichowatosha waliotangulia katika ummah huu kinawatosha waliokuja baada yao. Kilichowatosha waliotangulia kinatosha waliokuja baadaye. Nasaha na maelekezo bila kuhitaji kuigiza yanatosha.

Kwa hiyo washaurini watu na wanazuoni wanatoa nasaha na kuelekeza: hili ni halali, hili ni haramu, hili Allaah ameamrisha, hili Allaah amekataza na haya ni madhara yake na haya ni manufaa yake. Mtu afanye hivo kwa kubainisha na kufafanua. Hilo linatosha bila ya kuhitaji kuigiza. Mtu anajiweka kuwa ni fulani na fulani – anadanganya. Anajifanya kuwa ni ´Umar (Radhiya Allaahu ´anh) naye siyo ´Umar, anajifanya kuwa ni Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah naye si yeye, anajifanya kuwa ni Ibn ´Abd-is-Salaam naye si yeye, anajifanya kuwa ni ash-Shaafi´iy au Maalik naye si wao, anajifanya kuwa ni Abu Jahl, ´Utbah bin Rabiy´ah au Abu Lahab – anajiigiza kuwa makafiri – haya yote ni maovu.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/3179/حكم-تمثيل-ادوار-الصحابة-والعلماء-والاىمة
  • Imechapishwa: 26/10/2026