Swali: Mimi nilikula siku moja ya Ramadhaan na nikajiwa na siku ya tisa ambayo niliifunga pamoja na kuzingatia kwamba huifunga kila mwaka. Je, inatosheleza siku hiyo niliyokula?

Jibu: Haitoshelezi siku unayodaiwa ya Ramadhaan ukinuia kufunga Sunnah ya siku tisa. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Na kila mmoja atalipwa kwa kile alichonuia.”

Haitakikani kwake kufunga Sunnah ya siku tisa hali ya kuwa bado yuko na kitu katika Ramadhaan. Lakini akifunga siku tisa kwa nia kwamba analipa deni lake hakuna neno kwake kufanya hivo. Kuna matarajio akapata thawabu mara mbili; ujira wa kulipa na ufungaji wa siku hiyo. Ni kama ambavo endapo mtu ataingia msikitini akamkuta imamu anaswali na akajiunga pamoja nao katika swalah ya faradhi, basi anapata thawabu za kutekeleza faradhi na Tahiyyat-ul-Masjid. Jambo hili ni mfano wake. Akifunga siku ya tisa ya Dhul-Hijjah na akanuia pia kuwa analipa deni ya siku moja wapo anayodaiwa, itamtosheleza kutokamana na kulipa. Kuna matarajio ya kupata thawabu za siku hiyo. Kadhalika inahusiana na siku ya tisa na ya kumi za Muharram. Endapo mtu atazifunga na akanuia kuwa analipa pia, basi anapata yote mawili; kulipa deni lake na ujira wa kulipa siku mbili hizi.

Muulizaji: Iwapo atafunga kwa kunuia siku tisa za Dhul-Hijjah au tarehe tisa na kumi za mwezi wa Muharram. Swawm hiyo ni sahihi?

Ibn ´Uthaymiyn: Amenuia kufunga Sunnah?

Muulizaji: Ndio, amenuia kufunga Sunnah ilihali yuko na swawm ya wajibu?

Ibn ´Uthaymiyn: Wanachuoni wametofautiana juu ya masuala haya. Miongoni mwao wako ambao wanaona kuwa haijuzu kwa ambaye anadaiwa Ramadhaan kufunga Sunnah kabla yake. Wako wengine ambao wanaona kuwa inafaa kufunga Sunnah kabla yake. Hayo ni kwa sababu deni hili wakati wake ni mpana. Hivyo inafaa kwa mtu akaichelewesha mpaka Sha´baan mpaka pale kutapobaki kati ya deni hilo na Ramadhaan ya pili kwa kiwango cha siku anazodaiwa. Kwa hivyo wakati wake ukiwa ni mpana kufunga Sunnah kabla yake ni jambo linafaa.  Ni kama ambavyo inafaa kwa mtu kuswali swalah ya Sunnah kabla ya swalah ya faradhi ndani ya wakati wake. Bi maana inafaa kwa mtu kuswali swalah ya Sunnah kabla ya swalah ya Dhuhr kukiingia wakati wa Dhuhr na kuswali swalah ya Sunnah kabla ya swalah ya ´Aswr ukiingia wakati wa swalah ya ´Aswr. Kwa sababu wakati  ni mpana. Wakati ukiwa mfinyu kiasi cha kwamba hakukubaki katika Sha´baan isipokuwa kile kiwango anachodaiwa Ramadhaan, katika hali hii haifai kwake kufunga swawm ya Sunnah. Lakini muda wa kuwa muda ni mpana inasihi kufunga Sunnah. Lakini lengo litafikiwa pasi na makatazo yoyote akifanya yale niliyomtajia mwanzoni; bi maana anuie baadhi ya siku hizo kuwa anafunga pia madeni yake.

Muulizaji: Siku hizi tisa zinaweza kunijia na mimi sijatwahirika kutoka katika ada ya mwezi. Je, inafaa kwangu kulipa siku hizi baada ya siku tisa kupita?

Jibu: Hapana, asifunge hali ya kulipa. Kwa sababu hiyo ni siku maalum. Ikipita mapendekezo yake yamekwishapita. Akiifunga [huko mbeleni] hapati ujira wa siku hiyo. Huenda vilevile mtu akasema kuwa anapata ujira wake. Kwa sababu aliacha kufunga kwa sababu ya udhuru. Ni kama ambavo akiacha kufunga Ramadhaan kwa sababu ya udhuru basi atatakiwa alipe. Lakini kunahitajia kuangalia vizuri juu ya jambo hili. Kwa sababu kufunga Ramadhaan ni wajibu na ni lazima kwa watu kufunga. Ama siku zengine hizi zimependekezwa tu na mahali pake pamepita. Sunnah mahali pake pakipita inadondoka.

  • Mhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Nuur ´alaad-Darb (13) http://binothaimeen.net/content/6775
  • Imechapishwa: 26/01/2021