Ibn Baaz kuhusu kazi ya uanasheria

Swali: Ni nani wakili? Kazi yake ni nini? Hali yake ikoje?

Jibu: Wakili ni yule anayesimama mahali pa mwenye haki kudai haki yake na kumtetea. Ikiwa anadai haki ya kweli bila kuvuka mipaka ya Shari´ah, basi hana kosa. Lakini akidai yasiyo ya kweli kwa niaba ya mwenye madai, ambapo akasema uwongo na akapindukia mipaka, basi hushiriki katika dhuluma na uadui. Wakili au mpiganaji kesi anapaswa asivuke mipaka ya Shari´ah, bali ajitahidi kutafuta usahihi na haki. Aseme haki iwe kwa manufaa ya mteja wake au dhidi yake. Asipindukie mipaka kwa ajili ya kumpatia mteja wake kitu kisicho haki. Akiwa anapindukia, anasema uwongo, anaongeza maneno, anamdhulumu mwenye kudaiwa au kumtuhumu kwa batili ili kumpendeza mteja wake au kwa sababu ya pesa alizoahidiwa, basi huyu ni mwenza katika dhambi na uadui na ni dhalimu.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: https://binbaz.org.sa/fatwas/1007/حقيقة-مهنة-المحامي
  • Imechapishwa: 24/12/2025