Hukumu za safari kwa wenye kazi za udereva

Swali: Dereva anayesafiri kila siku, je, inajuzu kwake kufupisha swalah katika hali hii?

Jibu: Dereva na wengineo wakisafiri umbali wa kupunguza swalah – ambao ni takribani 80 km – basi inafaa kwao kufupisha swalah kwa kufuata mfano wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) na Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum). Ikiwa ataswali kwa ukamilifu pia hapana vibaya. Lakini akikaa katika mahali fulani kwa kukusudia kukaa zaidi ya siku nne, basi ataswali swalah kwa ukamilifu kwa mtazamo wa wanazuoni wengi. Vivyo hivyo ikiwa mtu yuko peke yake lakini kuna wenyeji wanaoishi hapo kwa kudumu, basi ataswali pamoja nao katika mkusanyiko na ataswali swalah kwa ukamilifu. Hatakiwi kuswali peke yake kwa ajili ya kufupisha swalah, kwa sababu kufupisha swalah ni Sunnah na kuswali kwa mkusanyiko ni wajibu. Hivyo wajibu hutangulizwa mbele ya Sunnah. Imethibiti kutoka kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kwamba msafiri akiswali pamoja na wenyeji wa mji, basi ni wajibu kwake kuswali swalah kwa ukamilifu.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (30/190)
  • Imechapishwa: 10/03/2026