Dalili juu ya ukafiri wa mwenye kuacha swalah zimetamkwa wazi ndani ya Qur-aan na Sunnah. Kutoka ndani ya Qur-aan amesema (Ta´ala):

فَخَلَفَ مِن بَعْدِهِمْ خَلْفٌ أَضَاعُوا الصَّلَاةَ وَاتَّبَعُوا الشَّهَوَاتِ ۖ فَسَوْفَ يَلْقَوْنَ غَيًّا إِلَّا مَن تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا

“Wakafuata baada yao waovu walipoteza swalah na wakafuata matamanio; basi watakutana na adhabu Motoni. Isipokuwa yule aliyetubu na akaamini na akafanya mema.”[1]

Ni dalili inayofahamisha kuwa pale alipoacha swalah na akafuata matamanio yake sio muumini. Vilevile amesema (Ta´ala):

فَإِن تَابُوا وَأَقَامُوا الصَّلَاةَ وَآتَوُا الزَّكَاةَ فَإِخْوَانُكُمْ فِي الدِّينِ

“Wakitubu na wakasimamisha swalah na wakatoa zakaah, basi ni ndugu zenu katika dini.”[2]

Ikafahamisha kuwa udugu katika dini hauwi isipokuwa kwa kusimamisha swalah na kutoa zakaah. Hata hivyo Sunnah ikafahamisha ya kuwa asiyetoa zakaah hakufuru muda wa kuwa anathibitisha kuwa ni wajibu hata hivyo akaacha kutoa kwa sababu ya ubakhili. Kwa msemo mwingine ni sharti kupatakane swalah ili kubakie ule udugu wa kiimani. Hiyo ina maana ya kwamba udugu wa kiimani unaondoka kwa kuacha swalah. Udugu hauondoki kwa dhambi au kufuru ndogo. Kwa sababu dhambi na kufuru ndogo haimtoi mwenye nayo nje ya udugu wa kiimani. Kama alivosema Allaah (Ta´ala) kuhusu makundi mawili ya waumini yanayopigana vita:

إِنَّمَا الْمُؤْمِنُونَ إِخْوَةٌ فَأَصْلِحُوا بَيْنَ أَخَوَيْكُمْ

“Hakika si vyenginevyo waumini ni ndugu, hivyo basi suluhisheni baina ya ndugu zenu.”[3]

Hata kama kumpiga vita muumini ni katika ukafiri, lakini hata hivyo makundi mawili hayo hayatoki katika udugu wa kiimani. Ibn Mas´uud (Radhiya Allaahu ´anh) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kumtukana muislamu ni dhambi nzito na kumpiga vita ni ukafiri.”[4]

[1] 19:59-60

[2] 9:11

[3] 49:10

[4] al-Bukhaariy (48) na Muslim (64).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/41-42)
  • Imechapishwa: 26/03/2026