Kuhusu masimulizi kutoka kwa Maswahabah (Radhiya Allaahu ´anhum), ´Umar bin al-Khattwaab (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Hakuna fungu katika Uislamu ambaye anaacha swalah.”[1]

´Abdullaah bin Shaqiyq amesema:

“Hakuna kitu Maswahabah wa Mtume wa Allaah ambacho walikuwa wakionelea kukiacha kwake ni kufuru isipokuwa swalah.”[2]

Ikiwa dalili ya kiwahy na ya kimapokezi inafahamisha juu ya ukafiri wa ambaye haswali, basi vivyo hivyo dalili ya kinadharia. Imaam Ahmad (Rahimahu Allaah) amesema:

“Kila ambaye anaichukulia wepesi na kuidharua swalah basi anauchukulia wepesi na kuudharua Uislamu. Fungu lao katika Uislamu ni kwa kulingana na fungu lao la swalah. Mapenzi yao ya Uislamu ni kwa kulingana na mapenzi yao ya swalah.”

Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

“Hakuna yeyote anayesadikisha kuwa Allaah ameamrisha swalah kisha akaendelea kuiacha swalah. Kwani ni jambo lisilowezekana kabisa kikawaida na kimaumbile akasadikisha kwa yakini kabisa kuwa Allaah amemfaradishia kila siku vipindi vitano vya swalah na kwamba atamuadhibu kwa kuziacha adhabu kali kabisa kisha baada ya hapo akaendelea kuiacha. Hili ni jambo lisilowezekana kabisa. Hakuna yeyote anayesadikisha ufaradhi wake kikweli ambaye anaendelea kuziacha, kwa sababu imani inamwamuru mswaliji kuziswali. Ikiwa moyoni mwa mtu hakuna kile kinachomwamrisha kuziswali, basi moyoni hakuna chochote katika imani. Usimsikilize yeyote ambaye hana uzoefu wala ujuzi hukumu na matendo ya moyo.”[3]

Amesema kweli katika yale aliyoyasema. Ni jambo lisilowezekana kabisa mtu akaacha swalah, pamoja na wepesi na urahisi wake, ukubwa wa adhabu yake na adhabu kwa kule kuiacha, kisha eti moyoni mwake kukawa kuna kitu katika imani.

[1] Ibn Abiy Shaybah (103). Swahiyh kwa mujibu wa al-Albaaniy ”Kitaab-ul-Iymaan” (103) cha Ibn Abiy Shaybah.

[2] at-Tirmidhiy (2622) na al-Haakim (1/7).

[3] Kitaab-us-Swalaah wa Hukmu Taarikihaa, uk. 400.

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/43-44)
  • Imechapishwa: 26/03/2026