Imebainishwa waziwazi ndani ya Qur-aan na Sunnah ya kwamba asiyeswali ni kafiri na ametoka katika Uislamu, ni haramu kwake kumuoa mwanamke wa Kiislamu. Uharamu huo umethibitishwa ndani ya Qur-aan, Sunnah na maafikiano. Allaah (Ta´ala) amesema:

وَلَا تَنكِحُوا الْمُشْرِكَاتِ حَتَّىٰ يُؤْمِنَّ ۚ وَلَأَمَةٌ مُّؤْمِنَةٌ خَيْرٌ مِّن مُّشْرِكَةٍ وَلَوْ أَعْجَبَتْكُمْ

“Na wala msiwaoe wanawake washirikina mpaka waamini. Na mjakazi Muumini ni bora kuliko mshirikina japo akikupendezeni.”[1]

Amesema (Ta´ala) kuhusu wale wanawake wanaohajiri:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِذَا جَاءَكُمُ الْمُؤْمِنَاتُ مُهَاجِرَاتٍ فَامْتَحِنُوهُنَّ اللَّـهُ أَعْلَمُ بِإِيمَانِهِنَّ ۖ فَإِنْ عَلِمْتُمُوهُنَّ مُؤْمِنَاتٍ فَلَا تَرْجِعُوهُنَّ إِلَى الْكُفَّارِ ۖ لَا هُنَّ حِلٌّ لَّهُمْ وَلَا هُمْ يَحِلُّونَ لَهُنَّ

”Enyi mlioamini! Wanapokujieni waumini wa kike waliohajiri, basi wajaribuni. Allaah anajua zaidi imani zao. Mkiwatambua kuwa ni waumini wa kike, basi msiwarejeshe [Makkah] kwa makafiri – wao si [wake] halali kwao [hao makafiri] na wala wao si [waume] halali kwao.”[2]

Waislamu wameafikiana juu ya yale yaliyojulishwa na Aayah hizi mbili na kwamba ni haramu kwa mwanamke wa Kiislamu kuolewa na mwanaume kafiri. Kutokana na haya mwanaume mwenye usimamizi akimuozesha mwanaume asiyeswali basi ndoa haisihi. Mwanamke huyu hawi ni halali kwake kwa ndoa hii, kwa sababu ni ndoa isiyoafikiana na amri ya Allaah na Mtume Wake (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam). Imethibiti kwamba ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Yeyote atakayefanya kitendo kisichokuwa ndani yake amri yetu atarudishiwa mwenyewe.”[3]

Ikiwa ndoa haisihi pale ambapo mume ataacha swalah, isipokuwa ikiwa kama atatubia na kurudi katika Uislamu kwa kuanza kuswali tena, tusemeje kuhusu kumuozesha mwanaume ambaye tangu hapo mwanzo haswali?

Kwa kumalizia ni kwamba ikiwa mchumba huyu haswali swalah ya mkusanyiko, ni fasiki na hakufuru, na inafaa kumuozesha, ingawa bora zaidi ni kumuozesha mwanamme ambaye yuko na dini na maadili mema. Ikiwa haswali kabisa, si swalah ya mkusanyiko wala peke yake, basi kafiri mwenye kuritadi aliyetoka katika Uislamu. Haifai kumuozesha mwanaume kama huyu mwanamke wa Kiislamu kwa hali yoyote isipokuwa ikiwa kama atatubia tawbah ya kweli, akaswali na akashikamana kisawasawa na Uislamu.

[1] 2:221

[2] 60:10

[3] Muslim (1718).

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/44-45)
  • Imechapishwa: 20/03/2026