Hadiyth kuhusu watu aina saba ni maalum kwa wanaume?

Swali: Je, Hadiyth kuhusu wale watu saba watakaofunikwa na Allaah chini ya kivuli siku ambayo hakutokuwa na kivuli isipokuwa kivuli Chake inawahusu wanamme peke yao au pia ambaye atafanya matendo kama ya watu hawa katika wanawake atapata thawabu za watu hawa zilizotajwa katika Hadiyth?

Jibu: Fadhilah hizi zilizotajwa katika Hadiyth sio kwa wanamme peke yao. Bali inawahusu wanamme na wanawake. Kijana wa kike ambaye amekulia katika kumwabudu Allaah ni mwenye kuingia katika hayo. Vivyo hivyo wanawake wenye kupendana kwa ajili ya Allaah ni wenye kuingia katika hayo. Hali kadhalika kila mwanamke ambaye aliitwa kwenye machafu na mwanamme mwenye nafasi ambapo akakataa kwa sababu ya kumcha Allaah ni mwenye kuingia katika hayo. Vivyo hivyo yule ambaye atatoa swadaqah inayotokana na chumo zuri na mkono wake wa kushoto usijue kile kilichotolewa na mkono wa kuume ni mwenye kuingia katika hayo. Aidha yule mwanamke ambaye atamkumbuka akiwa faragha ambapo akalia ni mwenye kuingia katika hayo kama wanamme.

Kuhusu kiongozi mwadilifu ni mambo maalum kwa wanamme. Vivyo hivyo swalah ya mkusanyiko msikitini ni katika mambo maalum kwa wanamme. Swalah ya mwanamke nyumbani kwake ndio bora zaidi kwake, kama ilivyopokelewa juu ya hilo Hadiyth ambazo ni Swahiyh kutoka kwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

  • Mhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (06/439)
  • Imechapishwa: 23/02/2021