Swali: Ni ipi hukumu ya mwanamke kuvaa mavazi ya kubana wakati anakuwa na jamaa zake  wa kiume wasioweza kumuoa?

Jibu: Kuvaa mavazi ya kubana ambayo yanaonyesha maungo yanayofitinisha ya mwanamke ni haramu. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kuna watu aina mbili wa Motoni sijawaona: wanaume walio na bakora kama mkia wa ng´ombe ambazo wanawapiga kwazo watu, na wanawake waliovaa vibaya, uchi, waliopinda na wanawapindisha wengine. Vichwa vyao ni kama nundu ya ngamia. Hawatoingia Peponi na wala hawatonusa harufu yake. Harufu yake inapatikana umbali wa kadhaa na kadhaa.”[1]

Waliovaa lakini bado wako uchi inaweza kufasiriwa ya kwamba wanavaa mavazi mafupi yasiyofunika vile viungo ambavyo inalazimika kuvifunika, ni mepesi kwa kiasi cha kwamba hayazuii kuona kile kilicho nyuma yake katika ngozi ya mwanamke au kwamba wanavaa mavazi yenye kubana kwa njia ya kwamba yanaonyesha yale maungo yanayofitinisha ya mwanamke. Kwa ajili hiyo haijuzu kwa mwanamke kuvaa mavazi kama haya yenye kubana isipokuwa mbele ya yule ambaye inafaa kwake kumuonyesha sehemu zake za kisiri – naye ni mume wake. Kwani hakuna sehemu ya siri baina ya mume na mke kwa sababu Allaah (Ta´ala) amesema:

وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ * إِلَّا عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أَوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ

“… ambao wanahifadhi tupu zao. Isipokuwa kwa wake zao au wale iliyowamiliki mikono yao ya kuume, basi hao si wenye kulaumiwa.”[2]

Hakuna sehemu ya siri kati ya mtu na mke wake. Kwa hivyo haijuzu kwa mwanamke kuvaa mavazi ya kubana yanayoonyesha yale maungo yanayofitinisha ya mwanamke si mbele ya wanawake wenzake wala ndugu zake wa kiume wasioweza kumuoa.

[1] Muslim (2128) na Ahmad (2/356).

[2] 70:29-30

  • Muhusika: Imaam Muhammad bin Swaalih bin ´Uthaymiyn
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (12/273)
  • Imechapishwa: 03/04/2026