Ameswali kwa kukamilisha baada ya kunuia kukaa zaidi ya siku nne

Swali: Nilikuwa katika safari London na mwanzoni sikukusudia kukaa kwa muda maalum na hivyo nikaswali swalah kwa kufupisha na kukusanya. Kisha nilipokusudia kukaa kwa muda fulani nikaswali swalah kwa ukamilifu. Ni ipi hukumu ya hilo?

Jibu: Uliyoyafanya ndiyo maneno ya jopo kubwa la wanazuoni  na jambo hili limenukuliwa kuwa ni maafikiano na Ibn-ul-Mundhir. Sunnah sahihi zimefahamisha kwamba msafiri anaruhusiwa kupunguza swalah katika safari. Vivyo hivyo ni jambo limewekwa katika Shari´ah kwake kukusanya swalah mbili pale sababu yake inapokuwepo ikiwa hakukusudia kukaa kwa muda maalum.

Ama ikiwa amekusudia kukaa kwa muda maalum unaozidi siku nne, basi anawajibika kuswali swalah kwa ukamilifu kwa mtazamo wa wanazuoni wengi. Baadhi ya wanazuoni wamesema kwamba inafaa kufupisha swalah muda wa kuwa hakukusudia kuishi kabisa katika mahali hapo, bali amekaa kwa sababu ya haja au dharura, na itakapomalizika atasafiri. Haya ni maneno yenye nguvu yanayothibitishwa na Hadiyth nyingi.

Kwa hali yoyote umefanya vizuri katika uliyoyafanya, kwa sababu uliposwali swalah kwa ukamilifu baada ya kukusudia kukaa kwa muda maalum unaozidi siku nne, umetoka katika makinzano ya wanazuoni na umefanyia kazi lililo salama zaidi.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (30/184)
  • Imechapishwa: 10/03/2026