Ambaye amerukuu hali ya kuwa imamu ameenda katika sijda ya kisomo

Swali: Imamu alifanya Takbiyr kisha akasujudu sijda ya kisomo. Lakini baadhi ya maamuma, khaswa wanawake, wakarukuu wakidhani kwamba amefanya Takbiyr ya Rukuu´ na hawakujua isipokuwa baada ya kuinuka kutoka katika sujuud. Ni nini kinawapasa? Na ni nini kinawapasa kama ikitokea kinyume chake, kwamba imamu akafanya Takbiyr ya kwenda katika Rukuu´ lakini baadhi ya maamuma wakasujudu sijda ya kisomo wakidhani kwamba imamu amesujudu sijda ya kisomo?

Jibu: Yule aliyerukuu wakati imamu yuko katika sijda ya kisomo na hakujua isipokuwa baada ya kuinuka, anatakiwa amfuate imamu katika sehemu iliyobaki ya swalah na hakuna kitu juu yake. Kwa sababu hakujua alichokifanya imamu. Vivyo hivyo kama imamu akirukuu na maamuma akadhani kwamba amesujudu, basi atasimama kutoka katika sijda. Akisimama kikamilifu atarukuu kisha atainuka, halafu atamfuata imamu wake katika sehemu iliyobaki ya swalah. Hakuna kitu juu yake, kwa sababu hakukusudia kwenda kinyume naye, bali hakujua kilichotokea.

  • Muhusika: Imaam ´Abdul-´Aziyz bin ´Abdillaah bin Baaz
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Majmuu´-ul-Fataawaa (30/169)
  • Imechapishwa: 08/03/2026