96. Hakuna imamu yeyote aliyewahi kusema kuwa Allaah hayuko mahali

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Hajapatapo yeyote katika wao siku hata moja kusema kuwa Allaah hayuko ndani ya ulimwengu, nje yake, amefungamana nao wala ametengana nao.

Hajapatapo yeyote katika wao siku hata moja kusema kuwa haifai kumuashiria kwa mkono na mfano wa hivo. Bali imethibiti katika “as-Swahiyh” kupitia kwa Jaabir bin ´Abdillaah (Radhiya Allaahu ´anhumaa) ya kwamba Mtume wakati alipotoa Khutbah yake kubwa siku ya ´Arafah katika mkusanyiko mkubwa uliodhuhuriwa na Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Je, nimefikisha?” Wakasema: “Ndio.” Ndipo akanyoosha kidole chake kuelekea mbinguni kisha akawaelekezea nacho na kusema: “Ee Allaah! Shuhudia!”

Alifanya hivo zaidi ya mara moja. Yako mengi mfano wa hayo.

MAELEZO

Hajapatapo yeyote katika wao siku hata moja kusema kama wanavosema Mu´attwilah, kwamba Allaah hana mahali kabisa na kwamba hayuko ndani wala nje ya ulimwengu, hayuko juu wala chini, hayuko kuliani wala kushotoni. Ahl-us-Sunnah wal-Jamaa´ah wanasema kuwa Allaah yuko juu na ametengana na viumbe Wake (Subhaanahu wa Ta´ala).

Wapingaji wa sifa wanakataza kuashiria kidole Kwake ili kutilia mkazo kuwepo Kwake juu ya viumbe. Lakini Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliashiria kidole Kwake wakati akitoa Khutbah, khaswa Khutbah ya kuaga na akasema:

“Je, nimefikisha?” Wakasema: “Ndio.” Ndipo akanyoosha kidole chake kuelekea mbinguni kisha akawaelekezea nacho na kusema: “Ee Allaah! Shuhudia!”

Huku ni kumuashiria Allaah kwamba yuko juu. Hakuashiria kuliani, kushotoni au upande wa chini ardhini. Jahmiyyah na wafuasi wao wanasema kuwa haijuzu kumuashiria Allaah, kwa sababu wao wanaona kuwa Hayuko upande wowote. Kwa maana nyingine Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alifanya jambo ambalo halijuzu kwa Jahmiyyah na wafuasi wao. Kiumbe mtukufu zaidi kwa kidole chake kitukufu zaidi aliashiria Kwake juu mbele ya mkusanyiko mkubwa, mkusanyiko wa waislamu ´Arafah, katika siku tukufu na maeneo patukufu. Kuna mifano mingi kama hiyo ya namna ambavyo Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) anamuashiria Mola wake juu ya mbingu. Hayawezi kudhibitiwa kihesabu wala hayawezi kukanushwa wala kupingwa.

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 138-139
  • Imechapishwa: 01/09/2024