86. Hakuna Hadiyth ambayo ni pigo kwao kama Hadiyth ya kijakazi

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah amesema:

Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema kumwambia kijakazi:

“Allaah yuko wapi?” Akajibu: “Juu mbinguni.” Akamuuliza tena: “Mimi ni nani?” Akajibu: “Wewe ni Mtume wa Allaah.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mwache huru. Kwani hakika ni muumini.”[1]

MAELEZO

Mu´aawiyah bin al-Hakam as-Sulamiy alighadhibika ambapo akampiga kofi kijakazi wake. Kisha akajuta kwa kumpiga na akataka kutoa kafara juu ya kitendo chake. Hivyo akataka kumwacha huru na akaenda kwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) kumuuliza juu ya jambo hilo. Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamjaribu na kumuuliza:

“Allaah yuko wapi?” Akajibu: “Juu mbinguni.” Akamuuliza tena: “Mimi ni nani?” Akajibu: “Wewe ni Mtume wa Allaah.” Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: “Mwache huru. Kwani hakika ni muumini.”

Wakati alipojibu kuwa Allaah yuko juu ya mbingu, ndipo (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akamthibitishia imani. Hapa kuna faida kubwa:

1 – Inafaa kuuliza ni wapi yuko Allaah, kwa sababu Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) alisema:

“Allaah yuko wapi?”

Bi maana upande gani. Swali hili linafaa na ni jambo ambalo mjinga anatakiwa kufunzwa.

2 – Anayemsifu Allaah kuwa juu ni muumini, na asiyemthibitishia Allaah (´Azza wa Jall) kuwepo juu ya mbingu ni kafiri. Hakuna Hadiyth ambayo ni pigo kwa Mu´tazilah kama hii. Wao wanaona kuwa haifai kuuliza ni wapi alipo Allaah. Kwa sababu wao wanaona kuwa Allaah yuko kila mahali au kwamba hana mahali; hayuko ndani, wala nje, wala kualini, wala kushotoni na kadhalika. Kwa msemo mwingine Hapatikani.

[1] Muslim (537), Abu Daawuud (930), an-Nasaa’iy (3/13), Maalik (2/776), Ibn Abiy ´Aaswim (479), al-Bayhaqiy, uk. 422, Ahmad (5/447) na Abu Daawuud at-Twayaalisiy (1105).

  • Mhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Ta´liyqaat at-Tawdhwiyhiyyah ´alaa Muqaddimat-il-Fatwaa al-Hamawiyyah, uk. 126-127
  • Imechapishwa: 26/08/2024