82. Kila kitambo kidogo Muumba yuko katika kazi

Kuona kwake kunakienea kila kitu kinachoonwa. Anaona mtembeo wa sisimizi mweusi juu ya jiwe gumu jeusi katika usiku wa giza totoro. Basi yaliyofichika Kwake ni dhahiri. Yale ya siri kwake ni ya wazi. Anajua siri na kilichojificcha zaidi ya siri. Siri ni kile kilicho ndani ya kifua cha mja na kilichopita moyoni mwake na hakijasemwa kwa midomo yake. Kilichofichika zaidi ya siri ni kile ambacho bado hakijapita moyoni, lakini Allaah anajua kwamba kitapita katika muda fulani.

Yeye ndiye Mwenye kuumba na kuamrisha. Yeye ndiye Mwenye ufalme na sifa njema. Yeye ndiye Mwenye dunia na Aakhirah. Yeye ndiye Mwenye neema, fadhilah na sifa njema. Ufalme wote ni Wake. Sifa njema zote ni Zake. Mikononi Mwake kuna kheri yote. Kwake ndiko kunarejea mambo yote. Uwezo Wake umekienea kila kitu. Rehema Yake imekienea kila kitu. Neema Zake zimefikia kila kilicho hai:

يَسْأَلُهُ مَن فِي السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ ۚ كُلَّ يَوْمٍ هُوَ فِي شَأْنٍ

”Wanamuomba Yeye wote walio mbinguni na ardhini, kila siku Yeye yumo katika kuleta jambo.”[1]

Husamehe dhambi, huondoa huzuni, hufichua dhiki, humtia nguvu aliyevunjika moyo, humtajirisha fakiri, humfundisha mjinga, humuongoza aliyepotea, humwelekeza aliyepotea njia, humsaidia mwenye dhiki, humkomboa mfungwa, humshibisha mwenye njaa, humvika aliye uchi, humponya mgonjwa, humrejeshea afya aliyejaribiwa, hukubali tawbah ya mwenye kutubu, humlipa aliyefanya mema, humsaidia aliyedhulumiwa, humuangamiza jabari, husitiri kosa, hufunika uchi, hulinda kutoka na khofu na huwainua watu na huwashusha wengine.

Halali kwake usingizi wala haustahiki kwake usingizi. Hushusha mizani na huiinua. Yanapandishwa Kwake matendo ya usiku kabla ya mchana na matendo ya mchana kabla ya usiku. Pazia Lake ni nuru; lau angeilifunua basi nuru ya uso Wake ingeziteketeza kila kitu kilichoifikia macho yake kutoka nyuma yake. Mkono Wake wa kuume umejaa; haupungukiwi na matumizi anayotoa usiku na mchana. Je, mmeona kile alichokitokea, tangu alivyoumba viumbe, pasi na kupungua chochote katika vile vilivyoko mkononi Mwake?

[1] 55:29

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 150-152
  • Imechapishwa: 01/09/2025