71. Wakati wa Twawaaf ya kuondoka

Anapotaka kuondoka, basi hatoki mpaka aiage Nyumba kwa kufanya Twawaaf ya kuaga baada ya kumaliza mambo yake yote, ili jambo lake la mwisho liwe ni Twawaaf ya kuaga kwenye Nyumba. Ikiwa baada ya hapo atajishughulisha na biashara, basi atairudia Twawaaf ya kuaga kwenye Nyumba.

Wakati wa kufanya Twawaaf ni jambo linalopendeza kusimama kati ya kona na mlango, aishikilie Nyumba na aseme:

اللهم هذا بيتك، وأنا عبدك، وابن عبدك، وابن أمتك، حمَّلتَني على ما سخَّرتَ لي من خلقك، وسيَّرتني في بلادك حتى بلَّغتني بنعمتك إلى بيتك، وأعنتَني على أداء نسكي، فإن كنتَ رضيتَ عني فازددْ عني رضًا، وإلا فمن الآن قبل أن تنأَى عن بيتك داري، فهذا أوانُ انصرافي إن أذنتَ لي، غير مستبدِلٍ بك ولا ببيتك، ولا راغبٍ عنك ولا عن بيتك، اللهم فأَصحِبْني العافيةَ في بدني، والصحةَ في جسمي، والعصمةَ في ديني، وأحسِنْ منقلَبي، وارزقني طاعتك  ما أبقيتَني، واجمعْ لي بين خيري الدنيا والآخرة، إنك على كل شيء قدير

“Ee Allaah! Hii ni Nyumba Yako na mimi ni mja Wako, mwana wa mja Wako na mwana wa mjakazi Wako. Umenibebesha juu ya kile ulichonirahisishia miongoni mwa viumbe Vyako na umenisafirisha katika nchi Zako mpaka kwa neema Yako umenifikisha katika Nyumba Yako na umenisaidia kutekeleza ´ibaadah yangu. Ikiwa umekuwa radhi nami, basi niongezee radhi Yako; na ikiwa hujaridhika nami, basi kuanzia sasa, kabla sijawa mbali na Nyumba Yako na makazi yangu, huu ndio wakati wa kuondoka kwangu, ikiwa utaniruhusu. Sijaweka mwingine badala Yako, wala badala ya Nyumba Yako, wala sitaki kukuacha Wewe wala Nyumba Yako. Ee Allaah! Nipe afya katika mwili wangu, afya njema katika mwili wangu na hifadhi katika dini yangu. Na ufanye mahali pangu pa kurejea kuwa pazuri na uniruzuku utiifu Wako muda wa kuwa utanihifadhi na nikusanyie mema ya dunia na Aakhirah. Hakika Wewe ni Muweza wa kila jambo.”

Halafu huomba kwa jambo analolitaka, kisha humswalia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam).

Mwenye kuondoka kabla ya kufanya Twawaaf ya kuaga, basi atarudi kuifanya ikiwa yuko karibu. Ikiwa yuko mbali, basi atatuma mnyama wa fidia.

Isipokuwa mwanamke mwenye hedhi na mwanamke mwenye damu ya uzazi – hakuna Twawaaf ya kuaga juu yao. Aida inapendekezwa kwao kusimama kwenye mlango wa msikiti na kuomba du´aa.

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 49
  • Imechapishwa: 11/11/2026