69. Alama itayomtambulisha Mola siku ya Qiyaamah

69 – Ibn Mas´uud amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

”Allaah atawakusanya wa mwanzo na wa mwisho wao katika Siku maalum. Watasimama kwa miaka arobaini huku macho yao yakikodoa juu mbinguni wakisubiri  kuhukumiwe. Allaah atashuka katika kivuli cha mawingu, kutoka kwenye ´Arshi kwenda katika Kursiy. Kisha aite mwitaji: ”Enyi watu! Hamridhiki na Mola wenu ambaye amekuumbeni na akakuruzukuni na akakuamrisheni mumwabudu Yeye na msimshirikishe na chochote kwamba kila mmoja achukue kile alichokuwa amechukua na alichokuwa akikiabudu ulimwenguni? Namna hiyo si ndio uadilifu kutoka kwa Mola wenu?” Waitike: ”Ndio.” Waondoke na wadhihirishiwe mfano wa vile walivyokuwa wakiviabudu. Wako watakaoliendea jua, wengine wataundea mwezi. Wale waliokuwa wakimwabudu ´Iysaa, watadhihirishiwa shaytwaan ´Iysaa, na wale waliokuwa wakimwabudu ´Uzayr, watadhihirishiwa shaytwaan ´Uzayr. Atabaki Muhammad na ummah wake. Ndipo ajidhihirishe Mola mbele yao, awaendee na kusema: ”Ni kwa nini hamwondoki kama walivyoondoka wengine?” Waseme: ”Sisi tuko na Mola ambaye bado hatujamuona.” Aseme: ”Mtamjua pindi mtapomuona?” Waseme: ”Ndio. Sisi tuko na alama kati yetu sisi na Yeye; tukiiona basi tutamtambua.” Ndipo Aseme: ”Ni alama ipi?” Waseme: ”Atafunua muundi Wake.” Hapo ndipo atafunua muundi Wake. Watu wote wenye migongo wataporomoka chini, ilihali watu wataokuwa na migongo kama pembe za ng´ombe nao watataka kusujudu lakini hawatoweza. Kisha Aseme: ”Inueni vichwa vyenu!” Awape nuru kutokana na matendo yao – na Mola (´Azza wa Jall) atakuwa mbele yao.”

Cheni yake ya wapokezi ni nzuri[1].

[1] Mambo ni kama alivosema nzuri, au pengine juu ya hapo zaidi. Ameitaja kwa ufupi kupitia njia nyingi za wapokezi, akiwemo ´Abdullaah bin Ahmad. Kisha yeye pia akaitaja kwa njia kamilifu zaidi kwa cheni yake yote ilioungana kwenda mpaka kwa Ibn Mas´uud. Imepokelewa kwa ukamilifu wake na ´Abdullaah bin Ahmad katika ”as-Sunnah”, uk. 177. Mtunzi amesema katika “al-Arba´iyn fiy Swifaati Rabb-il-´Aalamiyn” ya kwamba ni Swahiyh.

  • Mhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Ahmad adh-Dhahabiy
  • Mfasiri: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Mukhtasar-ul-´Uluww, uk. 110-111
  • Imechapishwa: 26/06/2024
  • taaliki: Imaam Muhammad Naaswir-ud-Diyn al-Albaaniy