Hii ni sehemu muhimu inayopaswa kuzingatiwa. Tambua kwamba zimekuja Hadiyth nyingi katika Swahiyh na nyinginezo zikionyesha kupendekezwa kuinua sauti juu katika kusoma. Sambamba na hilo yamekuja pia masimulizi yanayofahamisha kupendekezwa kusoma kwa sauti ya kimyakimya. Tutataja baadhi yake kwa ufupi kuashiria asili yake.

Imaam Abu Haamid al-Ghazaaliy na wengine miongoni mwa wanazuoni wamesema kwamba njia ya kukusanya baina ya Hadiyth na masimulizi haya tofauti ni kwamba kusoma kimyakimya ni mbali zaidi na kujionyesha. Kwa ajili hiyo ni bora kwa anayekhofia hilo. Ikiwa haogopi kujionyesha, basi kusoma kwa sauti ya juu ni bora, kwa sababu ndilo lililofanyiwa kazi zaidi na sababu nyingine manufaa yake yanawafikia wengine. Kinachowafikia wengine ni bora kuliko kinachojibana kwa mtu mwenyewe. Isitoshe huamsha moyo wa msomaji, hukusanya fikira zake, huelekeza usikivu wake, huondoa usingizi, huongeza uchangamfu na huamsha wengine waliolala au walioghafilika na kuwapa hamasa. Kwa hiyo atakapokusudia mojawapo ya nia hizi, basi kusoma kwa sauti ya juu huwa bora. Ikiwa nia hizi zitakusanyika, basi malipo huongezeka. al-Ghazaaliy amesema:

”Kwa sababu hiyo tumesema kwamba kusoma kwa kuangalia ndani ya msahafu ni bora.”

Namna hii ndivo ilivyo hukumu ya jambo hili.

  • Muhusika: Imaam Yahyaa bin Sharaf an-Nawawiy (afk. 677)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: at-Tibyaan fiy Aadaabi Hamalat-il-Qur-aan, uk. 66
  • Imechapishwa: 23/11/2026