62. Daima kinachozingatiwa ni wakati na pahali pa Dhikr

35 – Dhikr humsafirisha mja akiwa kitandani mwake, sokoni, hali ya afya au ugonjwa, neema au raha. Hakuna kitu kinachojumuisha nyakati na hali zote kama Dhikr. Mpaka humsafirisha mja akiwa amelala kitandani mwake ambapo akamtangulia mwenye kusimama kwa ghasia. Basi huyu huamka asubuhi na tayari amepita kundi zima naye amelala kitandani mwake. Na yule aliyekuwa hajitambui huamka akiwa nyuma ya msafara. Hiyo ni fadhilah ya Allaah humpa amtakaye. Imesimuliwa kutoka kwa mtu mmoja miongoni mwa wafanya ´ibaadah ambaye alimtembelea mtu kama mgeni. Yule mfanya ´ibaadah akasimama usiku wake wote akiswali na yule mtu mwengine akalala kitandani mwake. Walipoamka, yule mfanya ´ibaadah akamwambia: “Msafara umekuacha.” Akasema: “Suala si kwa ambaye ametumia usiku wake hali ya kusafiri na akaamka akiwa na msafara; suala ni kwa mtu ambaye ametumia usiku wake akiwa kitandani mwake na akaamka tayari keshaupita msafara.”

Hili na mfano wake lina maana sahihi na maana potofu. Basi mwenye kufasiri kwamba yule aliyelala kitandani mwake anamtangulia aliyesimama kwa ´ibaadah ni kosa. Maana yake sahihi ni kuwa huyu aliyelala kitandani ameshikamana na Mola wake (´Azza wa Jall) na akapachika upendo wa moyo wake katika ´Arshi. Akawa moyo wake unazunguka ´Arshi pamoja na Malaika, naye akawa amekosekana duniani na vilivyomo. Kilichomzuia kusimama usiku ni ugonjwa, baridi iliyomzuia asiinuke, khofu ya adui anayemtafuta au udhuru mwingine wowote. Basi huyu amelala kitandani mwake, na moyoni mwake mna yale ambayo Allaah (´Azza wa Jall) anayajua. Mwengine anasimama akiswali, akisoma na huku moyoni mwake mna kujionyesha, kujikweza na kutafuta sifa kwa watu. Au moyo wake uko sehemu moja na mwili wake uko sehemu nyingine. Basi bila shaka yule aliyelala huamka akiwa tayari amemtangulia huyu aliyesimama kwa hatua nyingi. Matendo hupimwa kwa nyoyo wala si kwa miili. Dhikr huchochea azimio lililotuama, huamsha upendo uliofichwa na hufufuliwa tamaa iliyokufa.

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 112-114
  • Imechapishwa: 21/08/2025