59. Maisha mazuri na yenye furaha ya Ibn Taymiyyah

Kumwelekea Allaah (Ta´ala), kurejea Kwake, kuridhika Naye na juu Yake na kujazwa moyo kwa mapenzi Yake, kushughulika kwa kumtaja Yeye, kufurahi na kufurahia kwa kumjua Yeye ni thawabu za haraka na Pepo ya sasa na ni maisha yasiyolinganishika kabisa na maisha ya wafalme. Nimemsikia Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) akisema:

”Hakika duniani kuna Pepo; yule asiyeingia humo basi haingii Pepo ya Aakhirah.”

Wakati fulani alinambia:

”Maadui zangu watanifanyia nini? Pepo yangu na bustani yangu imo kifuani mwangu. Nikihama basi imo pamoja nami haijitengani nami. Kunikamata ni upweke, kuniua ni shahaadah na kunitoa katika nchi yangu ni safari.”

Alikuwa akisema wakati amefungwa gerezani:

”Lau ningetoa dhahabu sawasawa na ujazo wa ukumbi huu, basi haingelingana kwangu na shukurani ya neema hii.

Au alisema:

”Sijawalipa kwa kile walichonisababishia katika wema.”

Alikuwa akisema katika Sujuud yake hali ya kuwa gerezani:

اللَّهُمَّ أَعِنِّي على ذِكْرِكَ وَشُكْرِكَ وَحُسْنِ عِبَادَتِكَ

”Ee Allaah! Nisaidie katika kukutaja, kukushukuru na kufanya vizuri ´ibaadah Yako.”

Wakati mmoja alinambia:

”Mfungwa ni yule aliyefungwa moyo wake na Mola wake (Ta´ala). Mateka ni yule aliyetekwa na matamanio yake.”

Alipoingia ndani ya ngome na akawa ndani ya ukuta wake aliiangalia na akasema:

فَضُرِبَ بَيْنَهُم بِسُورٍ لَّهُ بَابٌ بَاطِنُهُ فِيهِ الرَّحْمَةُ وَظَاهِرُهُ مِن قِبَلِهِ الْعَذَابُ

”Kisha utawekwa ukuta kati yao wenye mlango, ndani mna rehema na nje kwa upande wake wa mbele mna adhabu.”[1]

Naapa kwa Allaah kwamba sijaona kamwe mtu mwenye maisha mazuri kuliko yeye, licha ya kwamba alikuwa katika hali ya maisha magumu, kinyume na anasa na neema, licha ya kuwa katika kifungo, vitisho na mateso. Hata hivyo alikuwa miongoni mwa watu wenye maisha mazuri kabisa, wenye kifua kipana, wenye moyo imara, wenye roho yenye furaha. Nuru ya neema ilikuwa ikionekana usoni mwake. Tulikuwa tunaposhikwa na khofu kali, dhana mbaya kututawala na dunia ikawa finyu kwetu, basi tulikuwa tukimjia. Si lolote isipokuwa tukimwona na kusikia maneno yake, basi yote hayo huondoka na hubadilika kuwa faraja, nguvu, yakini na utulivu. Ametakasika kutokana na mapungufu Yule ambaye amewaonyesha waja Wake Pepo Yake kabla ya kukutana Naye! Akawafungulia milango Yake katika nyumba ya matendo ambapo akawapa kutokana na pumzi yake, upepo wake mtamu na harufu yake nzuri, kilichowafanya watumie nguvu zao zote kuitafuta na kushindana kuiendea.

[1] 57:13

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 108-110
  • Imechapishwa: 14/12/2025