Ni wajibu kufanya Hajj na ´Umrah mara moja katika maisha kwa muislamu mwenye akili timamu, aliyebaleghe na aliye huru, ikiwa ana uwezo wa kuifikia. Uwezo ni kuwa na chakula cha safari na kipando pamoja na mahitaji yake yanayofaa kwa mtu wa mfano wake, ziada ya yale anayohitaji kwa kulipa deni lake, matumizi yake mwenyewe na matumizi ya wale anaowalisha kwa kudumu.

Kwa mwanamke inashurutishwa kuwepo kwa Mahram wake, ambaye ni mume wake au yule ambaye ni haramu kwake kumuoa milele kwa nasaba au kwa sababu inayoruhusiwa.

Yule mwenye kupuuza mpaka akafa, basi hutolewa katika mali yake gharama ya Hajj na ´Umrah kwa niaba yake.

Hajj ya kafiri na mwendawazimu si sahihi. Ni sahihi kwa mtoto na mtumwa, lakini haiwatoshelezi. Na ni sahihi kwa mtu asiye na uwezo na kwa mwanamke bila Mahram.

Mwenye kumfanyia mwingine Hajj, hali ya kuwa hajawahi kujifanyia Hajj mwenyewe, hajawahi kutekeleza Hajj ya nadhiri yake au Hajj ya kujitolea kwake, na akaifanya kabla ya Hajj ya Uislamu, basi Hajj yake itahesabika kuwa ni Hajj ya faradhi yake mwenyewe, wala si ya mwingine.

  • Muhusika: Imaam Muwaffaq-ud-Diyn bin Qudaamah al-Maqdisiy (afk. 620)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: ´Umdat-ul-Fiqh, uk. 44
  • Imechapishwa: 05/11/2026