5 – Hakimu wa Hijr Salmayah bin ´Aaswim amesema:

“Bishr al-Mariysiy alimuandikia barua Mansuur bin ´Ammaar akimuuliza kuhusiana na maana ya maneno Yake (Ta’ala):

الرَّحْمَـٰنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَىٰ

”Mwingi wa rehema amelingana juu ya ´Arshi.”[1]

Akamwandikia kumjibu: “Kulingana Kwake hakuna kikomo na kuuliza juu yake ni kujikakama. Kuulizia kwako hilo ni Bid´ah na ni wajibu kuyaamini yote hayo. Amesema (Ta’ala):

فَأَمَّا الَّذِينَ فِي قُلُوبِهِمْ زَيْغٌ فَيَتَّبِعُونَ مَا تَشَابَهَ مِنْهُ ابْتِغَاءَ الْفِتْنَةِ وَابْتِغَاءَ تَأْوِيلِهِ

”Basi wale ambao katika nyoyo zao mna upotevu hufuata zile zisizokuwa wazi ili kutafuta fitina na kutafuta kuzipotosha.”[2]

6 – Abu ´Aliy al-Husayn bin al-Fadhwl al-Bajaliy aliulizwa kuhusu ni namna gani amelingana juu ya ´Arshi Yake ambapo akajibu:

”Mimi siyajui yaliyofichika isipokuwa tu yale tuliyobainishiwa. Yeye (‘Azza wa Jall) ametufundisha kwamba amelingana juu ya ´Arshi Yake na wala hakutujuza amelingana juu vipi.”[3]

7 – al-Khatwiyb al-Baghdaadiy amesema:

”Kuhusu sifa zilizotajwa ndani ya Sunnah sahihi, ´Aqiydah ya Salaf (Radhiya Allaahu ‘anhum) juu yake ni kuzithibitisha na kuzipitisha katika udhahiri wake na kuzikanushia kuzifanyia namna na kuzifananisha. Maudhui haya yamejengeka kwamba kuzungumzia Sifa ni kama kuzungumzia Dhati mia kwa mia.

Iwapo inajulikana vyema kwamba kumthibitisha Mola (‘Azza wa Jall) ni kuthibitisha uwepo Wake, sio kuthibitisha ukomo wala namna, basi vivyo hivyo kuthibitisha sifa Zake ni kuthibitisha uwepo Wake, na sio kuthibitisha namna wala namna.

Tukisema kwamba Allaah (Ta´ala) ana mkono, usikivu na uoni, ni sifa ambazo Allaah (Ta´ala) amejithibitishia Mwenyewe. Wala hatusemi kwamba maana ya mkono ni uwezo au kwamba maana ya kuona na kusikia ni ujuzi. Wala hatusemi kuwa ni viungo vya mwili wala kuzifananisha na mikono, masikizi na maono ambavyo ni sehemu za mwili na vyombo vya utendaji. Tunasema kwamba ni lazima kuzithibitisha, kwa sababu wahy umezitaja kwa njia ya kuzithibitisha. Sambamba na hayo ni lazima kuzikanushia ufanano, kwa sababu Yeye (Tabaarak wa Ta´ala) amesema:

لَيْسَ كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖوَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ

“Hakuna chochote kinachofanana Naye – Naye ni Mwenye kusikia yote, Mwenye kuona yote.”[4]

وَلَمْ يَكُن لَّهُ كُفُوًا أَحَدٌ

“Na wala hana yeyote anayefanana [na kulingana] Naye.”[5]

[1] 20:05

[2] 3:7

[3] ´Aqiydat-us-Salaf wa Asw-hhaab-il-Hadiyth, uk. 40.

[4] 42:11

[5] 112:4

  • Muhusika: Shaykh ´Abdur-Razzaaq bin ´Allaamah ´Abdil-Muhsin al-´Abbaad al-Badr
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Athar al-Mash-huur ´an-il-Imaam Maalik fiy Swifat-il-Istiwaa’, uk. 76-77