50. Mwanadamu anahitaji kumtaja Allaah

Allaah (Ta´ala) amesema:

فَإِذَا قَضَيْتُم مَّنَاسِكَكُمْ فَاذْكُرُوا اللَّـهَ كَذِكْرِكُمْ آبَاءَكُمْ أَوْ أَشَدَّ ذِكْرًا

“Mtakapomaliza kutekeleza ‘ibaadah za hajj zenu, basi mtajeni Allaah kama mnavyowataja baba zenu au mtajeni zaidi.”[1]

Hii ni amri ya kufanya Dhikr kwa wingi kwa sababu mja anahitaji sana kumtaja Allaah na hawezi kujitosheleza bila ya Dhikr hata kwa jicho la mda mfupi. Basi wakati wowote ambao mja amepita bila ya kumtaja Allaah (´Azza wa Jall), basi ni hasara kwake na ni hasara kubwa zaidi kuliko chochote alichokipata katika kusahau kwake kwa Allaah. Baadhi ya watambuzi wamesema:

“Lau mja angemwelekea Allaah (Ta´ala) kwa miaka kadhaa kisha akamgeukia kwa muda mfupi, basi aliyokosa ni makubwa zaidi kuliko aliyoyapata.”

al-Bayhaqiy amesimulia kutoka kwa ´Aaishah (Radhiya Allaahu ´anhaa) ambaye amesimulia kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Hakuna saa yoyote inayompitia mwanadamu bila kumtaja Allaah isipokuwa ataijutia siku ya Qiyaamah.”[2]

Amesimulia vilevile kutoka kwa Mu´aadh bin Jabal ambaye ameeleza kuwa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Kitu pekee watachojutia watu wa Peponi ni kuhusu saa iliyowapitia bila ya kumtaja Allaah (´Azza wa Jall) ndani yake.”[3]

Umm Habiybah, mke wa Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam), ameeleza ya kwamba Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) amesema:

“Maneno yote ya mwanadamu ni dhidi yake si kwa faida yake – isipokuwa kuamrisha mema, kukataza mabaya au kumdhukuru Allaah (´Azza wa Jall).”[4]

Mu´aadh bin Jabal (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

”Nilimuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam): “Ni matendo yepi yanayopendwa zaidi kwa Allaah (´Azza wa Jall)?” Akasema: “Ufe huku ulimi wako ni mbichi kwa kumtaja Allaah (´Azza wa Jall).”[5]

Abud-Dardaa´ (Radhiya Allaahu ´anh) amesema:

“Kila kitu kina kisafishaji. Hakika kisafishaji cha nyoyo ni kumtaja Allaah (´Azza wa Jall).”

[1] 2:200

[2] Shu´b-ul-Iymaan (2/408-209). Nzuri kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Swahiyh-ul-Jaamiy´” (5720).

[3] Shu´b-ul-Iymaan (2/408-209). Cheni yake ya wapokezi ni nzuri kwa mujibu wa al-Mundhiriy katika “at-Targhiyb wat-Tarhiyb” (2/375), dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf-ut-Targhiyb wat-Tarhiyb” (910).

[4] at-Tirmidhiy (2412), aliyesema kuwua Hadiyth ni nzuri na ngeni, Ibn Maajah (3974) na al-Haakim (1/512-513). Dhaifu kwa mujibu wa al-Albaaniy katika “Dhwa´iyf Sunan at-Tirmidhiy” (2412).

[5] at-Twabaraaniy (20/107-108). Swahiyh kwa mujibu wa Ibn Hibbaan (818) na nzuri kwa mujibu wa Ibn Hajar katika “Nataa-ij-ul-Afkaar” (1/92).

  • Muhusika: Imaam Shams-ud-Diyn Muhammad bin Abiy Bakr bin Qayyim-il-Jawziyyah (afk. 751)
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: al-Waabil as-Swayyib wa Raafi´-ul-Kalim at-Twayyib, uk. 89-91
  • Imechapishwa: 17/08/2025