50. Aliyefariki akiwa na deni la swawm ya wajibu

Ikiwa atafariki aliyekuwa na deni la ulipaji kabla ya kuingia Ramadhaan mpya, basi hakuna chochote juu yake. Kwa sababu alikuwa na ruhusa ya kuchelewesha katika kipindi alichofariki. Ikiwa atafariki baada ya Ramadhaan mpya, basi ikiwa kuchelewesha kulikuwa kwa udhuru, kama ugonjwa au safari, mpaka ikamkuta Ramadhaan mpya, basi hakuna chochote juu yake pia. Ikiwa kuchelewesha kulikuwa pasi na udhuru, basi kafara ni wajibu itolewe katika mali yake kwa kumlisha chakula masikini mmoja kwa kila siku aliyochelewesha.

Ikiwa atafariki aliyekuwa na swawm ya kafara, kama swawm ya kafara ya mwanaume aliyemfananisha mke wake na mama yake au swawm iliyo wajibu kwa fidia ya damu ya Tamattu´ katika Hajj, basi atalishiwa masikini mmoja kwa kila siku wala hafungiwi kwa niaba yake. Chakula hicho kitatolewa katika mali yake, kwa sababu ni swawm isiyokubali uwakala katika uhai, basi ndivyo ilivyo baada ya kifo, jambo ambalo ndio msimamo kwa kikosi kikubwa cha wanazuoni.

Ikiwa atafariki aliyekuwa na swawm ya nadhiri, basi inapendekezwa kwa walii wake amfungie. Hilo ni kutokana na yale yaliyothibiti kwa al-Bukhaariy na Muslim kwamba:

”Mwanamke mmoja alimjia Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) akasema: ”Hakika mama yangu amefariki na juu yake kuna swawm ya nadhiri. Je nifunge kwa niaba yake?” Akasema: ”Ndio.”[1]

Walii ni mrithi. Imaam Ibn-ul-Qayyim (Rahimahu Allaah) amesema:

”Nadhiri hufungiwa kwa niaba yake bila swawm ya faradhi ya msingi, jambo ambalo ndio maoni ya Ahmad na wengineo na ndicho kilichopokelewa waziwazi kutoka kwa Ibn ´Abbaas, ´Aaishah na ndiyo yanayoashiriwa na kipimo. Kwa sababu nadhiri si wajibu kwa msingi wa Shari´ah, bali mja ndiye aliyejilazimisha juu ya nafsi yake na hivyo ikawa kama deni. Ndiyo maana Mtume (Swalla Allaahu ´alayhi wa sallam) aliifananisha na deni.”

Ama swawm ambayo Allaah ameifaradhisha tangu mwanzo, basi ni nguzo miongoni mwa nguzo za Uislamu na hivyo haiingii uwakala kwa hali yoyote. Ni kama ambavyo swalah na shahaadah havikubali uwakala. Kwa sababu lengo lake ni utiifu wa mja kwa nafsi yake mwenyewe na kusimama kwake kwa haki ya ´ibaadah aliyoumbiwa na kuamrishwa, jambo ambalo haliwezi kutekelezwa na mtu mwingine kwa niaba yake na wala hakuna anayeswali kwa niaba ya mwingine.

Shaykh-ul-Islaam Ibn Taymiyyah (Rahimahu Allaah) amesema:

”Hulishwa kwa niaba yake masikini mmoja kwa kila siku iliyompita. Hivyo ndivyo alivyoona Ahmad, Ishaaq na wengineo. Hii ndiyo inayoashiriwa na mtazamo wa kielimu, kama ilivyo wajibu wa athari. Kwa hakika nadhiri ilikuwa imethibiti katika dhimma na hivyo hutekelezwa baada ya kifo. Ama swawm ya Ramadhaan, basi Allaah hakuifaradhisha kwa asiyeweza kuitekeleza. Bali alimwamrisha asiyeweza kutoa fidia ya kumlisha masikini. Ulipaji ni kwa yule anayeweza, si kwa yule aliyeshindwa. Hivyo hakuna haja ya mtu kumlipia mwingine. Ama swawm ya nadhiri na mengineyo miongoni mwa yaliyolazimishwa kwa nadhiri, basi hufanyiwa kwa niaba yake bila maoni tofauti kwa mujibu wa Hadiyth Swahiyh.”

[1] al-Bukhaariy (1953) na Muslim (1148).

  • Muhusika: Imaam Swaalih bin Fawzaan al-Fawzaan
  • Tarjama: Firqatunnajia.com
  • Marejeo: Ithaaf Ahl-il-Iymaan bi Duruus Shahri Ramadhwaan, uk. 46-47
  • Imechapishwa: 19/03/2026